Profesa Kabudi Atema Cheche Dodoma......Akerwa na maamuzi kufanyika bila Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuarifiwa.
WAZIRI
wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuanzia sasa
mawakili walioko kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wanasheria wote
katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za Serikali
watakuwa ni Mawakili wa Serikali.
Ametoa
kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Agosti 15, 2018) kabla hajamkaribisha
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ahutubie wageni waliohudhuria uzinduzi wa
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
“Kwa
miaka mingi kumekuwa na ombwe la usimamizi wa wanasheria walio kwenye
utumishi wa umma. Maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika pasipo Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu kuwa na taarifa. Mambo yanapoharibika ndio Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali inataarifiwa ili kuokoa jahazi,” alisema.
Alisema
hali hiyo kwa miaka mingi imekuwa ikiisababishia Serikali kuingia
kwenye migogoro na kuingia hasara. “Baada ya mabadiliko haya, wanasheria
wote walioajiriwa katika utumishi wa umma wanakuwa wanafanya kazi na
kutumia mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya wizara zao,
taasisi zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa,” alisema.
“Vilevile
wanasheria hao watakuwa chini ya uangalizi wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali. Nia ya mabadiliko haya ni kumuwezesha Mwanasheria Mkuu wa
Serikali awe na usimamizi juu yao na kuwazuia kufanya kazi bila kufuata
maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”
Prof.
Kabudi alisema mashirika yote ya kimkakati kama vile Bandari, TANESCO
nayo pia yataletwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili
kuepuka kuitia Serikali hasara. “Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye
mashirika haya, lakini kuna maamuzi yanafanyika wakati Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu haina taarifa,” amesema.
“Kutokana
na marekebisho hayo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaratibu
na kusimamia Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi hiyo na wanasheria
wote katika Wizara, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za Serikali
ambao sasa watakuwa ni Mawakili wa Serikali. Aidha, Mawakili wa Serikali
walio katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali watakuwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mkurugenzi wa
Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali,” amesema.
Amesema
marekebisho hayo yanatokana na marekebisho ya muundo wa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia matangazo ya Serikali Na. 48, 49 na
50 ya tarehe 13 Februari, 2018.
“Leo
tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya marekebisho hayo. Rais
alianzisha Ofisi huru ya Taifa ya Mashtaka kuchukua nafasi ya iliyokuwa
Divisheni ya Mashtaka chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Vilevile, Rais alianzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ajili ya
kutekeleza majukumu ya usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai
yakiwemo ya kikatiba ambayo Serikali ni mdaawa ambayo awali yalikuwa
yakishughulikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema.
Amesema
marekebisho hayo yanakusudia kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa
mashtaka ya jinai nchini hususani utekelezaji wa azma ya Serikali ya
kutenganisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.
“Kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kunalenga kuimarisha
usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai na pia kuiwezesha Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuimarika katika weledi na ubobezi wa
kitaalamu katika kuishauri Serikali na kuandika Miswada ya Sheria kwa
kuzingatia mabadiliko makubwa katika tasnia ya sheria kitaifa, kikanda
na kimataifa,” ameongeza.
Hata
hivyo, Prof. Kabudi alionya kwamba mabadiliko yoyote hayawezi kuleta
matokeo yaliyokusudiwa kama watendaji hawatabadili mtizamo wao. Ni kweli
muundo uliobadilishwa ulikaa kwa miaka mingi na inawezekana mambo mengi
yalikuwa yanafanyika kwa mazoea. “Kutokana na mabadiliko haya, tunakiri
kuwa mitizamo yetu na ya watumishi wenzetu lazima ibadilike.
Tumejipanga kuhakikisha kuwa watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea ili
wasiwe na tashwishwi wala ajizi katika kutekeleza majukumu ya umma.”
“In
public service, learn to swallow your pride. In public service, learn
to learn your limits. In public service, learn to obey the authority
above you, and if you don’t, resign and quit,” alisisitiza.
“Tumejipanga
kufanya kazi kwa weledi na katika hili tutaweka mikakati ya kuwaongezea
watumishi wa ofisi hizi ujuzi katika maeneo mahususi, na katika hilo
tutaweka mipango ya kuwafanyia placement ndani na nje ya nchi ili wapate
ujuzi mahususi na kuhakikisha wanapata mafunzo ya muda mfupi na mrefu
katika maeneo mbalimbali.
Alisema
wameanza mkakati wa kuanzisha umoja wa wanasheria walio katika utumishi
wa umma ili kuwawezesha kukutana mara kwa mara na kwamba Agosti 30-31
mwaka huu, wanatarajia kufanya mkutano huo ili kuwaunganisha wanasheria
wote wajione wanafanya kazi moja na katika Serikali moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.
Mpekuzi.
Comments