Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umesema matukio ya kupigwa na
kuteswa kwa raia wakiwa mikononi mwa polisi yanaongezeka siku hadi siku
na kuongeza hofu kwa jamii juu ya uwapo wa utawala wa sheria.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa THRDC,
Onesmo Olengurumwa, alisema matukio hayo yanaongezeka huku baadhi ya
watu wakitishwa na kuambiwa siyo raia na wengine kunyang'anywa pasi za
kusafiria.
Alisema
wanalaani vikali vitendo vya karibuni vya ukiukwaji wa sheria na haki
za waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu kunakofanywa na
Jeshi la Polisi lenye wajibu wa ulinzi wa raia na mali zao.
"Tunashuhudia
waandishi wakipigwa na kukamatwa na polisi wakati wakitekeleza majukumu
yao ya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi," alisema.
Alisema
kuwa Agosti 8, mwaka huu, mwandishi wa habari wa Wapo Radio, Silas
Mbise, alishambuliwa na kukamatwa na polisi akiwa kazini na alipigwa
waziwazi na polisi wenye silaha huku akiwa amelala chini na hana silaha
yoyote.
Alisema
kuwa tukio lingine la hivi karibuni ni la mwandishi wa gazeti la
Tanzania Daima, Sitta Tuma, aliyepigwa na kukamatwa na maofisa wa polisi
wakati akichukua habari katika mkutao wa kampeni za uchaguzi wa diwani
wilayani Tarime mkoani Mara.
"THRDC
ilitoa msaada wa kisheria ili kumwezesha kupata dhamana na wakili wake
Ernest Muhagama alisema alipofika polisi alielezwa kwa mtuhumiwa huyo
kakamatwa kwa kosa la kuandamana kinyume cha sheria. Aliachiwa kwa
dhamana Agosti 9," alisema.
Aliyataja
matukio mengine ni ya miezi miwili iliyopita dhidi ya wa waandishi wa
habari kuwa ni yaliyofanywa dhidi ya George Ramadhani na Christopher
Gamaina, waliokamatwa na polisi mkoani Mwanza wakati wakiwa wanatekeleza
majukumu yao na walifunguliwa mashtaka mahakamani.
Alisema
mwandishi mwingine ni Emmanuel Kibiki aliyekamatwa na polisi mkoani
Iringa na kulazimishwa kulala polisi kwa siku kadhaa kabla ya kufikishwa
mahakamani.
"Kwa
ujumla, hali ya uhuru wa wanahabari na vyombo vya kawaida na vya
mitandaoni umezidi kutoweka na kupelekea kuzuia Watanzania kupata habari
sahihi na kwa wakati kwa mujibu wa Katiba," alisema.
'Kwa sasa, wanahabari wamejawa na hofu kubwa kutoa taarifa zozote watakazohisi hazitawafurahisha baadhi ya watawala," alisema.
"Tunasikitishwa
na kuongezeka kwa matukio ya kupigwa na kukamatwa kwa wanahabari bila
sababu za msingi na za kisheria. Wanafanya kazi katika mazingira magumu
kutokana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na polisi," alisema.
Kwa
mujibu wa Olengurumwa, polisi ni chombo muhimu kinachotakiwa kusimamia
uhuru na usalama wa waandishi wa habari na siyo kuwashambulia kama
ilivyotokea mara kadhaa kwa baadhi ya maofisa wa polisi kutumia nguvu
kubwa kuwashambulia na kuwajeruhi wanahabari wakiwa kazini.
"Ni
lazima ikumbukwe kuwa kila mtu anayo haki ya ulinzi kwa mujibu wa
sheria za nchi, vyombo vya dola vina wajibu wa kuwalinda raia na mali
zao ikiwemo waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu
Tanzania," alisema.
Aliongeza
kuwa matukio ya watu kuhojiwa uraia wao yanazidi kuongezeka na sasa
wamefika viongozi na raia saba wanaodaiwa siyo raia licha ya kuzaliwa na
kuishi Tanzania kwa maisha yao yote.
Aliwataja
viongozi hao kuwa ni pamoja na Askofu wa Jimbo la Ngara, Severine
Niwemugizi, Olengurumwa, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania,
Abdul Nondo, Mkurugenzi wa Twaweza na Aidan Eyakuze.
Wengine
ni Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), Maanda
Ngoitiko na Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia
Kakobe.
"Matukio
kama haya yakiendelea kutokea hasa dhidi ya watetezi wa haki za
binadamu, yataendelea kusababisha hofu na kupoteza uhuru wa watetezi wa
kufanya kazi zao kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi," alisema na
kuongeza:
"Matumizi
ya nguvu kupita kiasi na kutojali utawala wa sheria pia vimezidi
kuchangia kuzorota kwa hali ya watetezi wa haki za binadamu nchini.
"Baadhi
ya vyombo vya dola vinatumia nguvu kubwa kuingilia uhuru wa asasi za
kiraia na watetezi wanapotaka kufanya mikutano ya ndani na kudai kuwa
lazima wawe na vibali au hali ya usalama hairuhusu mikutano hadi ya
ndani."
Mpekuzi.
Comments