Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka
amesema hataki kusikia wakuu wa wilaya zilizopo katika Mkoa wake
wakiwaweka ndani watumishi wa umma.
Mtaka
ametoa kauli hiyo Ijumaa Agosti 17, 2018 wakati akifunga kikao cha
madaktari wa mikoa na wilaya zote nchi nzima uliofanyika mjini Dodoma.
“Sisi
viongozi tuwalinde watumishi wetu, mimi nilipoenda kuwa mkuu wa mkoa wa
Simiyu niliwaambia wakuu wangu wa wilaya kuwa sitaki kusikia mtumishi
wa umma kuwekwa mahabusu,” amesema Mtaka.
“Wakati
mwingine ukiona matamko ya wanasiasa kwenye maeneo ya kazi unajiuliza
hivi RM0 (mganga mkuu wa mkoa) anakaa kwenye kikao kushauri haya
yatokee? Kwenye mkoa wangu hutaona huu upuuzi.”
Agosti
14, 2018 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alikemea tabia ya baadhi ya wakuu wa
wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo kuwaweka watu ndani.
Aliwataka wakuu hao kuhakikisha wanasoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ili kufanya kazi kwa weledi.
Katika
siku za hivi karibuni, wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia ‘sheria ya
saa 48’ kutoa adhabu kwa kuwaweka baadhi ya watu mahabusu.
Mamlaka
hiyo wamepewa kupitia Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 na
hutakiwa kutumia amri ya kumweka ndani-kwa muda usiozidi saa 48-mtu au
kundi la watu ambao kubaki kwao nje kunaweza kusababisha madhara
makubwa katika jamii.
Baadhi
ya viongozi hao wamekuwa wakitumia sheria hiyo kama adhabu au hukumu,
badala ya malengo yaliyowekwa ya kulinda usalama wa watu wengine.
Mpekuzi.
Comments