Mkuu Mpya wa mkoa wa Mbeya ajiapiza kumng'oa Sugu jimboni 2020......Awataka wanaCCM Wavunje Makundi.
Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu
wa Mkoa huo, Amos Makalla huku akijiapiza kuwa yuko tayari kutumbuliwa
na Rais kama viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo,
hawatakubali kuondoa makundi na kupoteza tena Jimbo la Mbeya Mjini.
Chalamila
alitoa kauli hiyo wakati wa makabidhiano hayo jana na kudai kuwa kwa
mtazamo wake anaona jimbo hilo kwa sasa lipo wazi na linaweza kurejea
katika himaya ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
CCM
ililipoteza kwa mara ya kwanza jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka
1995, Polisya Mwaiseje (NCCR-Mageuzi) alipomshinda Bruno Mpangala,
lakini ikalirejesha mwaka 2000 kupitia kwa Benson Mpesya.
Mwaka 2010, Mpesya aliangushwa na Joseph Mbilinyi 'Sugu' (Chadema) anayeendelea kuliongoza hadi sasa.
Katika
makabidhiano hayo, Chalamila alisema kuwa pamoja na mtazamo wake huo wa
uwezekano mkubwa wa kulirejesha CCM jimbo hilo, wanachama wa CCM
wasishangae kushindwa tena ikiwa wataendelea na makundi makubwa yaliyo
ndani ya chama hicho.
Alisema
amekuwa akifuatilia migogoro ya CCM Mbeya tangu alipokuwa Iringa na
amebaini kuna makundi makubwa ambayo yanaweza kukigharimu chama hicho.
“Endapo
nitaondolewa kwa sababu ya CCM kupoteza jimbo hili, nitarudi kulima,
nitamshukuru Rais na nitamwambia kuwa sijasikitika," Chalamila alisema
na kuongeza:
"Kama mtataka ushirikiano wa kujenga, mimi kama kamisaa wa chama, nitawapa lakini kama ni ushirikiano wa kuvurugana sitawapa."
Aliongeza
kuwa msimamo wake ni kufanya kazi bila kuingiliwa na kiongozi yeyote na
yeyote atakayetaka kuingilia majukumu yake atamtaka kusoma katiba na
miongozo ya chama.
Chalamila
alimshauri Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Jacob Mwakasole na timu
yake kuhakikisha wanapambana na kuyaondoa mapema makundi yaliyokivuruga
chama hicho.
Alisema kuwa atakuwa tayari kutoa ushauri na kama wataona ushauri wake haufai, atawaacha na hatawaingilia katika uamuzi wao.
Kiongozi
huyo wa serikali aliongeza kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Mkoa Mbeya
wamefarakanishwa kwa itikadi za kisiasa zilizokuwa zinasababishwa na
baadhi ya viongozi.
Alimpongeza
Makalla kwa jitihada alizozionyesha kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi
katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, hasa Mbarali na Rungwe.
Awali,
Makalla ambaye amehamishiwa Mkoa wa Katavi, alimweleza Chalamila kuwa
katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne, alikuwa anapambana na
migogoro ya ardhi ambayo ndiyo ilikuwa changamoto kubwa mkoani humo.
Alisema
baadhi ya migogoro alishaimaliza ikiwamo ya wananchi waliohamishwa
wakati wa upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Wananchi hao walikuwa
wanalalamika kupunjwa malipo ya fidia.
“Nakuhakikishia
kuwa tumeshirikiana na wakuu wa wilaya pamoja na viongozi wengine
wakiwamo wa dini kumaliza baadhi ya changamoto, lakini nitakukabidhi
baadhi ya migogoro ya ardhi kwa maandishi ili uendelee kuitatua,”
alisema.
Makalla
aliwataka wananchi na viongozi wa Mbeya kumpa ushirikiano Chalamila
kama walivyofanya kwake wakati akiuongoza mkoa huo unaosifika kwa
uzalishaji wa nafaka.
Mpekuzi.
Comments