Watendaji
wote ndani ya Jeshi la Magereza wametakiwa kujiandaa kisaikolojia
kupokea mkakati maalum wa uzalishaji wa chakula unaolenga kujitosheleza
kwa chakula cha wafungwa na ziada kuuzwa katika sehemu nyingine.
Hayo
yamesemwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Phaustine
Kasike jana Agosti 13, 2018 alipokuwa akizungumza na maafisa, askari na
watumishi raia wa jeshi hilo alipofanya ziara yake ya kwanza mkoani
Dodoma tangu ateuliwe kushika wadhifa huo Julai 13 mwaka huu.
Kamishna
Jenerali Kasike amesema maandalizi ya mkakati huo yanaendelea vizuri
makao makuu ya jeshi hilo na katika kipindi kifupi kijacho maelekezo ya
utekelezaji wake yatatolewa na kushushwa katika vituo vyote vya magereza
kwa ngazi ya mikoa na wilaya.
Amesema
mkakati huu utakapokuwa umekamilika itakuwa ndiyo dira ya utekelezaji
ndani ya jeshi na utamtaka kila kiongozi kuwa na mpango kazi katika
eneo lake unaokwenda sambamba na malengo mapana ya jeshi hilo.
“Ninaamini
jambo hili linawezekana na kwa kuanza na raslimali chache zilizopo
kwakuwa wataalam wapo, ardhi ipo na nyenzo za kuanzia zipo tukijipanga
vizuri tunaweza kupata mahala pazuri pa kuanzia” Amebainisha Jenerali
Kasike
Na
kuongeza “ miongoni mwa taasisi zenye wasomi wazuri katika maeneo
mengi ni pamoja na jeshi letu la Magereza, sasa umefika wakati wa kuona
wataalam hawa wanatumika kwa kushirikikshwa ipasavyo ili kuona wanaleta
tija jeshini na taifa kwa ujumla”
Sanjari
na hayo Kamishna Kasike amewataka watumishi wa jeshi hilo kote nchini
kubadili mtazamo wa namna wanavyofanya kazi kwa kusoma alama za nyakati
na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Kamishna
Kasike amesema ifike mahala kila mmoja ajisikie aibu na fedheha kuona
jeshi letu linasemwa vibaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake
ipasavyo hata katika mambo ambayo yako ndani ya uwezo wa watendaji
wenyewe.
Akitolea
mfano wa uingizwaji wa vitu visivyoruhusiwa magereza kama vile simu,
bangi, pesa nakadhalika kutohitaji bajeti kuviondoa ni kiasi cha
watendaji kubadilika tu.
“
Hapa kuna tatizo kubwa la kimaadili, badilikeni. Nitakuwa mkali sana.
Nimeanza kwa kuwaeleza ili nieleweke vizuri kwa hatua nitakazozichukua
kwa askari asiyetaka kubadilika. Adhabu zitakuwa kali kwelikweli.
Amesisitiza Jenerali Kasike.
Amewakumbusha
askari wote nchini kutambua dhamana waliyonayo, thamani ya kazi yao na
dhamana walizonazo kwa familia zao ili kuachana na tamaa zisizokuwa na
msingi ambazo mwisho huwaingiza katika matatizo makubwa.
Aidha,
Kamishna Kasike amewaambia kuwa anatambua uwepo wa changamoto kadhaa
kama vile ukosefu wa nyumba na zilizopo kuchakata, ukosefu mkubwa wa
vyombo vya usafiri, malimbikizo ya madeni, kutopandishwa vyeo kwa
wakati, uhaba wa sare na mengine.
Amewahakikishia
kuwa serikali iliyoko madarakani inayatambua yote na tayari imeanza
kuchukua hatua katika baadhi ya mambo na kuwaomba ushirikiano wakati
yeye akiwa mtendaji mkuu anafanya ufuatiliaji.
Ziara
ya Kamishna Kasike mkoani Dodoma imemfikisha pia gereza Msalato ambapo
ametembelea mradi wa upigaji kokoto na kuzungumza na maafisa na askari
wa gereza hilo. Awali alimtembelea Katibu Mkuu Utumishi Dr.Laurean
Ndumbaro ofisini kwake na kubadilisha taarifa mbalimbali za kiutendaji.
Mpekuzi.
Comments