Hatimaye
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amejibu mapigo ya
taarifa zilizokuwa zimesambaa kuwa anawatanguliza watu CCM ili baadaye
ahamie.
Akizungumza
mwishoni mwa wiki iliyopita katika jimbo la Monduli, Lowassa
alikanusha vikali taarifa hizo akidai kuwa wanaoeneza taarifa hizo ni
waongo na wambea.
Mbunge
huyo wa zamani wa Monduli ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani alimjibu
aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga akimtaka aweke wazi
sababu zilizomfanya ahame kwakuwa ni haki yake ya kikatiba bila kutumia
jina lake kwa uongo.
“Waambieni
waache umbea na uongo. Anasema uongo kwa kinywa chake. Mimi
nimtangulize kwani mimi sina miguu?” alisema Lowassa huku akisisitiza
kuwa hana mpango huo.
“Wanasema
eti mimi nimekubaliana na Magufuli kuwahamisha wabunge kwenda CCM.
Acheni kunichonganisha na Rais, mimi sina mpango wowote na [Rais]
Magufuli,” alisema.
Aliongeza
kuwa kinachofanywa na wanaohama ni haki yao na wanapaswa kuwaeleza
ukweli wananchi kuwa ni shida zao binafsi. Aidha, alimvaa Kalanga akidai
kuwa alikuwa na mikopo ambayo imelipwa na kumfanya ahame.
Lowassa
ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa miaka 20, aliwataka wananchi hao
‘kumtoa tongotongo’ kwenye uchaguzi wa Ubunge wa marudio akiahidi kuwa
angerejea hapo kwa ajili ya kufanya kampeni za ubunge.
Aliwataka
wananchi wa eneo hilo kupuuzia taarifa kuwa hakuna maendeleo ambayo
yanafanyika Monduli akiwataka kukumbuka maendeleo ambayo waliyashuhudia
alipokuwa mbunge.
Mwanasiasa
huyo mkongwe aliwahakikishia wana Monduli kuwa bado yuko imara kwenye
kambi ya upinzani na kuwataka kutoyumba huku akitolea mfano Nigeria
ambako wanasiasa takribani 600 wamehama vyama vyao. Alisema suala la
kuhama vyama ni la kawaida kwa wanasiasa hivyo lisiwashtue bali
liwafanye wawe imara zaidi.
Joto
la uchaguzi wa Ubunge Monduli limeanza kupanda baada ya aliyekuwa
mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Julius Kalanga kujiuzulu na
kujiunga na CCM kisha kuchukua fomu ya kugombea tena.
Chadema
ambao watakuwa na kibarua cha kutetea jimbo hilo wako katika hatua za
kuwachuja walioomba kugombea akiwemo Freddy ambaye ni mtoto wa Lowassa.
Mpekuzi.
Comments