JPM ateua wakurugenzi wapya 41 wa halmashauri.



Katibu Mkuu kiongozi, balozi John KijaziRais John Magufuli amefanya uteuzi wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri wapya 41 huku akiwahamisha wengine 19 katika vituo mbalimbali.
Akitangaza orodha ya majina ya wakurugenzi hao leo Jumatatu Agosti 13, 2018 Ikulu jijini Dar es Salaam,  Katibu Mkuu kiongozi, balozi John Kijazi amesema wakurugenzi wote wapya wanatakiwa kuripoti siku ya Jumatano, Agosti 15, 2018 katika ofisi za Katibu Mkuu wa Tamisemi.
“Wakurugenzi ambao katika mabadiliko haya wamebadilishwa vituo vya kazi, wanapaswa kwenda kuripoti katika vituo vyao vya kazi mara moja,” amesema.
“Kwa wale wakurugenzi walioteuliwa kwa mara ya kwanza wanatakiwa kuripoti kwa katibu mkuu wa Tamisemi siku ya Jumatano kwa ajili ya kiapo cha uadilifu na maelekezo ya majukumu yao.”
Balozi Kijazi amesema watakapokwenda Dodoma wanapaswa kuwa na vyeti vyao vya kidato cha nne, kidato cha sita na elimu ya taaluma.
Amesema kwa wale wakurugenzi ambao vituo vyao havikutajwa katika mabadiliko hayo wanapaswa kuendelea na nafasi zao katika vituo walivyopo sasa.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), kapteni mstaafu George Mkuchika amemteua Mkondwe Bendera kuwa katibu tawala mpya wa wilaya ya Rungwe ili kujaza nafasi iliyokuwa wazi kutokana na aliyekuwapo kupangiwa kazi nyingine.
Mwananchi.

Comments