Hakimu ahoji upelelezi kesi ya vigogo wa madini kutokamilika.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeubana upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya almasi kutaka Agosti 21, 2018 kueleza hali halisi kuhusu upelelezi wa kesi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Agosti 13, 2018 na hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri baada ya wakili wa Serikali mwandamizi,  Kishenyi Mutalemwa kudai kuwa wapo mbioni kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo na kumtaka wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko na wateja wake kuwa wastahamilivu.
Kishenyi ameiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kesi hiyo kwa ajili ya kutajwa na kwamba, upande wa mashtaka hauna lengo la kuwatesa washtakiwa bali kuwalinda.
Kwa upande wa wakili Nkoko, amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea, hawaelewi nia ya upande wa mashtaka ni nini.
Nkoko amedai  kesi hiyo imefunguliwa kwa ajili ya kuwatesa washtakiwa kwa kuwa kila wanapojaribu kufanya maombi ya dhamana upande wa mashtaka lazima wazuie.
Amedai kuwa hati ya mashtaka inaonyesha kila kitu ikiwa ni pamoja na kiwango cha hasara kinachodaiwa kusababishwa na washtakiwa, kwamba hajui ni upelelezi gani ambao wanaufanya.
“Tunaomba leo upande wa mashtaka wapewe nafasi na tarehe ijayo waeleze hali halisi ya upelelezi katika kesi hii,” amesema Nkoko.
Washtakiwa  katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji  Madini ya Almasi na Vito Tanzania (Tansort),  Archard Karugendo na Mthamini Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu ambao ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini.
Karugendo na Rweyemamu wanasota mahabusu kutokana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuzuia dhamana zao.
Wanakabiliwa na  kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4bilioni.
Wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.48bilioni ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.
Washtakiwa hao wanadaiwa  kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathaminishaji wa almasi wa Serikali na waajiriwa wa wizara hiyo waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 1,118,291.43  ambazo ni sawa na Sh 2.48bilioni.
mwananchi.

Comments