Dk. Shein aipongeza BoT.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuvutiwa na mafanikio makubwa yaliofikiwa na Benki kuu ya Tanzania (BoT), hasa katika kuhakikisha uchumi wa Tanzania hauyumbi.


Dk. Shein aliyasema hayo alipofanya mazungumzo na uongozi wa hiyo ulioongozwa na Gavana Prof. Florens Luoga uliofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.
Dk. Shein alisema jitihada kubwa zimechukuliwa na (BoT) ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha uchumi na kuunga mkono juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa uchumi wa Zanzibar na ule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uko vizuri na umekuwa ukiimarika ambapo miongoni mwa wanaochangia mafanikio hayo ni BoT.
Aliongeza kuwa mikakati na juhudi zinazochukuliwa na Benki hiyo hivi sasa katika kuhakikisha mzunguko wa fedha unakuwepo hasa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ni jambo la busara na litasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza maendeleo ya uchumi wa Tanzania na wananchi wake.
Aidha, alisema kuwa mikakati na juhudi za BoT ni vyema zikajikita katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii kwa upande wa Zanzibar ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Zanzibar.
Dk. Shein alisisitiza kuwa BoT ni ya wananchi wote wa Tanzania hivyo ni vyema wakafaidika na huduma za Benki hiyo ambayo imepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwake.
Sambamba na hayo, aliueleza uongozi huo kuwa mafanikio yote hayo iliyoyapata yanatokana na uwajibikaji mzuri katika utendaji wa kazi unaotekelezwa ndani ya benki hiyo.
Zanzibarleo.

Comments