Balozi Seif aikaribisha kiuwekezaji Holding Group.

KAMPUNI ya kimataifa ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group ya Dubai, imesema kuwa imevutiwa na mazingira ya Zanzibar, hivyo itawekeza miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Meneja mkuu wa Uhusiano wa kimataifa wa kapuni hiyo, Abdo Ali Kayali alieleza hayo jana akiwa na ujumbe wake wakati walipotembelea na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi huko ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Meneja huyo alisema uongozi wa kampuni hiyo umeridhika na fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar, sambamba na kuvutiwa na ukarimu mkubwa walionao watu wa visiwa vya Zanzibar vitu ambavyo vimeipa shauku kampuni hiyo kutaka kuwekeza miradi yake ya kiuchumi.
Kayali, alisema katika kuunga mkono jitihada za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye uimarishaji wa uchumi, taasisi hiyo imeonesha nia ya kuwasilisha maombi ya kutaka kuwekeza miradi katika sekta mawasiliano, uvuvi wa bahari kuu, kilimo na viwanda.
Alieleza kwamba kamuni hiyo yenye wataalamu wazoefu inaiangalia Zanzibar katika mtazamo wa kuijengea uwezo wa kutoa huduma za kibiashara katika eneo zima la mwambao wa Afrika Mashariki.
Akitoa shukrani za ujio wa ujumbe huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema sekta zilizopendekezwa na uongozi huo katika uwekezaji tayari serikali imeshazijengea mazingira bora ya miundombinu.
Balozi Seif aliutaka uongozi wa Kampuni hiyo kuwasiliana na viongozi wa taasisi husika nchini ili kupata muda wa kutosha wa kujifunza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo hapa nchini.
Zanzibarleo.

Comments