Malalamiko
ya muda mrefu ya wakulima yaliyokuwepo kwamba ushirika unatoa bei
ndogo, sasa yamepatiwa muarobaini baada ya serikali kupitia kwa kina
gharama za uendeshaji na uongezaji thamani kwa zao la kahawa kwa Vyama
vikuu vya ushirika Mkoani Kagera.
Serikali
imepiga marufuku kwa vyama hivyo vya ushirika kutoza zaidi ya shilingi
490 kwa kilo moja ya Kahawa ya maganda kama gharama za uendeshaji na
uongezaji thamani, Awali maainisho ya gharama hizo yalikuwa ni makubwa
ambapo kiasi cha shilingi 1350 kwa kilo moja ya Kahawa ya maganda
ilianishwa kama gharama za uendeshaji.
Waziri
wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba ameeleza agizo hilo jana 12 Julai
2018 wakati akizungumza na wajumbe wa Halmshauri kuu ya Chama Cha
Mapinduzi Mkoa wa Kagera kwenye Hoteli ya Bukoba Coop ambapo miongoni
mwa ajenda ya kikao hicho ilikuwa ni kujadili kuhusu soko la Kahawa na
uendeshaji wa ushirika.
Dkt
Tizeba amewaeleza wajumbe hao kuwa amepiga marufuku hiyo kufuatia
malalamiko ya wadau wa Kahawa Mkoani Kagera ambapo gharama hizo
zilionekana kuwa kubwa ukilinganisha na gharama halisi.
"Ndugu
zangu wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM inawezekanaje shilingi mia
mbili inatozwa kama ushuru wa chama kikuu, na shilingi mia mbili tena
inatozwa kama ushuru wa chama cha msingi, ni nani anaweza kukupa faida
namna hii sasa rasmi ushuru huu tumeupunguza kama nilivyoeleza"
Alikaririwa Mhe Tizeba
Aliongeza
kuwa swala la ushirika ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi
ambayo ni mkataba kati ya wananchi na serikali katika kipindi cha miaka
mitano kuanzia 2015-2020 kwa imani kubwa kwamba ndicho chombo pekee
kitakacho mkwamua mkulima na changamoto anazo kabiliana nazo kwenye
Kilimo na masoko ikiwa ni pamoja na kujiondoa katika umasikini.
Aidha,
Dkt Tizeba aliwaeleza wajumbe hao kuwa vyama vya ushirika havipaswi
kuendeleza mazoea ya kujiwekea gharama bila kwanza kutazama kipato cha
mkulima huku akieleza kuwa amewaelekeza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi
ambapo Wilaya zao zinalima Kahawa kote nchini kufuatilia kwa karibu
mwenendo wa masoko ya Kahawa kuanzia inavyokusanywa mpaka wakati
inapouzwa.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Bi
Costansia Buhiye amempongeza Waziri huyo wa kilimo kwa kujibu kero namba
10 ya kikao cha Halmshauri kuu ya CCM kuhusu wasiwasi wa bei ya kahawa
na namna na uendeshaji wa ushirika.
Buhiye
alimpongeza Waziri huyo kwa kutatua kadhia mbalimbali za wakulima wa
Kahawa katika ziara yake ya siku tatu Mkoani humo huku akieleza kuwa ana
imani kubwa sasa kuwa wajumbe hao watatembea kifua mbele endapo
wakulima wao watapatiwa bei nzuri.
Mpekuzi.
Comments