Waziri Wa Biashara Na Ushirika-Uganda Avutiwa Na Uendeshaji Ushirika Nchini Tanzania ....Aomba Ridhaa Kuja Kujifunza Nchini Tanzania.
Serikali
ya Uganda imeeleza kuvutiwa na uendeshaji wa ushirika nchini Tanzania
hivyo imeomba kupata ridhaa ya kuzuru nchini Tanzania ili kujifunza
namna bora ya uendeshaji wa ushirika.
Ombi
hilo limetolewa Julai 11, 2018 na Waziri wa Biashara na Ushirika
nchini Uganda Mhe Fredrick Ngobi Gume wakati akizungumza kwenye mkutano
uliohudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe
Charles Mwijage uliofanyika katika eneo la Mtukula Wilayani Misenyi.
Katika
mkutano huo Waziri huyo anayeshughulikia Ushirika nchini Uganda
alimpongeza Waziri wa Kilimo nchini Mhe Dkt Charles Tizeba kwa Nazi
kubwa aliyoifanya katika kipindi cha muda mfupi kurejesha imani kubwa na
ushirika kwa wakulima ambapo alimpongeza pia kwa tuzo ya heshima
aliyokabidhiwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa kwa
niaba ya wana ushirika wakati wa sherehe za kilele cha siku ya ushirika
Duniani kwenye viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza.
Waziri
wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Gume alimuhakikishia mwenyeji
wake kuwa biashara ya Kahawa nchini humo ina changamoto sawa katika
nchi zote mbili kwa kuwa swala la mikopo isiyo rasmi inayowanyonya
wakulima (Butura) nchini Uganda ipo kwa kiwango cha juu.
Alisema
kuwa serikali ya Uganda inayoongozwa na Rais wa nchi hiyo Mhe Yoweri
Kaguta Museveni itaendeleza ushirikiano na serikali ya Tanzania
inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli hivyo panapohitajika
ushirikishwaji katika biashara hususani kwenye sekta ya Kilimo watakuwa
na msimamo wa pamoja.
Alisema
miongoni kwa mambo mengine ya kujifunza nchini Tanzania itakuwa ni
pamoja na kujifunza kuhusu namna bora ya kuendesha ushirika na
kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani.
Kwa
upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alimueleza Waziri
Gume kuwa njia mojawapo ya kusimamia ushirika ni pamoja na mkakati wa
usimamizi madhubuti ikiwa ni pamoja na kuwaweka kizuizini wabadhilifu
wote katika ushirika.
Mkutano
huo ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati
akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 2
Julai 2018 na kuitaka Wizara ya Kilimo kufuatilia kwanini wakulima wa
zao la Kahawa wanacheleweshewa malipo yao sambamba na kujua kwanini
wakulima wanauza Kahawa yao nchini Uganda.
Naye
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage aliongeza
kuwa wakulima wa Tanzania na Uganda wanapaswa kuweka msisitizo katika
Kilimo kwani kufanya hivyo kutaongeza uimara na uanzishwaji wa viwanda
vitakavyoongeza chachu ya ajira kwa wananchi.
Mpekuzi.
Comments