WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma, Bw.
Raphael Mbwambo afuatilie ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe, baada ya kutilia shaka
makadirio ya ujenzi huo.
Amesema
mbali na ujenzi wa ofisi hiyo ambayo msingi wake ulikadiriwa kutumia sh
milioni 205 lakini Halmashauri imetumia zaidi ya sh, milioni 400, pia
halmashauri hiyo imeweka makadirio makubwa ya ujenzi wa hospitali ya
wilaya ambayo utekelezaji wake ni mgumu.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo jana (Jumatatu, Julai 30, 2018) wakati
akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Buhigwe pamoja na wananchi wa
wilaya hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya
wilaya hiyo inayojengwa kwenye eneo la Ruheta.
“Kamanda
wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma fuatilia ujenzi wa jengo la ofisi ya
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buhigwe na tunataka tujue ni nani
aliyetengeneza makadirio hayo kwa sababu makadirio aliyoyafanya ni
makubwa ulinganisha na mradi husika,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema “Hospitali mnayojenga ni ya kawaida, haiwezekani mkaweka
makadirio kama hayo ya kujenga wodi moja kwa sh milioni 851 wakati kuna
baadhi ya maeneo nchini Serikali imetumia sh. milioni 500 kujenga kituo
cha afya chenye majengo zaidi ya matano,”.
Kufuatia
hatua hiyo , Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kupitia upya
makadirio waliyoyaweka katika miradi mbalimbali ya ujenzi
wanayoitekeleza kwa kuwa makadirio waliyoyaweka ni makubwa na
yatakwamisha miradi yao.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka wakuu wa idara wahakikishe wanasimamia vizuri
majukumu ya idara zao na kuyatekeleza ipasavyo. “kila mtumishi wa wilaya
hii awajibike kwenye eneo lake na si vinginevyo,”.
Awali,
akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Brigedia
Jenerali, Marco Gaguti alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo ya wahamiaji haramu, ambapo kwa kipindi cha mwaka
mmoja wamekamata wahamiaji haramu 1,054.
Mkuu
huyo wa wilaya alisema zoezi la kuwasaka wahamiaji hao limesaidia kwa
kiasi kikubwa kupunguza uharifu pamoja na matukio ya utekaji wa kutumia
silaha unaofanywa na raia wa nchi jirani wanaoingia nchini kinyume cha
taratibu kwa kushirikiana na wananchi wasiokuwa waaminifu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Mpekuzi.
Comments