Waziri Mkuu Azindua Kampeni Ya Kufufua Zao La Michikichi.....Lengo ni kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amezindua kampeni ya kufufua zao la michikichi
mkoani Kigoma na kuagiza kuanzishwa kwa kituo cha utafiti wa zao hilo
katika chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga kilichopo mkoani Kigoma
kwa kuwa ndiko zao la Michikichi linalimwa kwa wingi.
Amesema
Serikali imedhamiria kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta ya
kula nchini kwa kuhamasisha kilimo cha zao la michikichiki kwa sababu
kila mwaka Serikali hutumia zaidi ya sh. bilioni 600 kwa ajili ya
kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo jana (Jumamosi, Julai 28, 2018) wakati akizungumza
na viongozi wa mkoa wa Kigoma, wadau wa zao la michikichi na wabunge wa
mkoa wa Kigoma baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya
siku nne inayolenga kuhamasisha maendeleo na kilimo cha zao la
Michikichi.
Amesema
Serikali haiwezi ikaendelea kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza
mafuta ya kula kutoka nje wakati uwezo wa kulima michikichi na kuzalisha
mafuta ya mawese kwa wingi tunao, hivyo amewataka viongozi wa Serikali
wabadilike na wawafuate wakulima kwenye maeneo ya vijijini na
wakawasimamie na kuwashauri namna bora ya kulima zao hilo.
Aidha,
ameagiza Wizara ya Kilimo ianze taratibu za kisheria za kukihamisha
chuo cha Kihinga kutoka Wizara ya Elimu Sayansi ya Teknolojia kwenda
wizara ya Kilimo ili shughuli za tafiti za zao la michikichi lifanyike
kwa ufanisi.
Pia,
ameiagiza Wizara ya Kilimo kuwahamishia mkoani Kigoma watumishi wa
kituo cha utafiti wa michikichi cha Bagamoyo ifikapo mwezi Agosti, 2018
isipokuwa wale wanaohusika na utafiti wa zao la minazi tu.
Kadhalika,
amewataka viongozi wa mikoa yote inayolima michikichi waanzishe
mashamba ya michikichiki ili waoneshe mfano kwa wananchi. “Serikali
inataka kuona mabadiliko kwenye zao hili. Sioni umuhimu wa Taifa
kuendelea kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi wakati uwezo wa
kuzalisha ndani upo,”.
Amesema
Serikali inataka kuona mabadiliko ya zao hilo, hivyo amewaagiza maafisa
ugani katika maeneo yote wanayolima zao hilo wakafualitie maendeleo ya
zao hilo kwa ukaribu zaidi. Zao hili litasimamiwa kuanzia hatua za
uandalizi wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na utafutaji wa masoko.
Waziri
Mkuu amewataka wananchi wote wa mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa mingine
inayolima michikichi, wahakikishe wanapanda michikichi kwa wingi kuanzia
kwenye makazi yao na kwenye mashamba yote wanayolima mazao mengine ili
kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
“Serikali
imefanya maamuzi ya kumaliza tatizo la mafuta ya kula nchini, kila
mmoja lazima awajibike katika kuinua zao la michikichi ili tuweze
kuzalisha mafuta ya kutosha,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itafuatilia kwa umakini kuhakikisha zao la
michikichi linalimwa kwa wingi na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa
ujumla. “Tutumie zao hili kama fursa ya kujikwamua na umasikini pamoja
na maliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini,”.
AwaliNaibu
Waziri wa Kilimo, Bw. Omary Mgumba alisema zao la mchikichiki ni muhimu
katika ukuzaji wa uchumi wa nchini, hivyo ufufuaji wa zao hilo ni
kichocheo cha viwanda kwa kuwa kutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa
malighafi, hivyo kuvutia wawekezaji.
Amesema
kiasi kikubwa cha zao hilo hutumika katika kuzalisha mafuta ya kula,
sabuni, hivyo ameshauri kiwepo chuo cha utafiti wa zao la michikichi
mkoani Kigoma ili kurahisisha shughuli za uzalishaji. Mafuta yatokanayo
na zao la michikichi yana mahitaji makubwa kwa kuwa bei yake ni nafuu
jambo linalowezesha watu wengi wakiwemo wa hali ya chini kuyatumia.
Kwa
upande,wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel
Maganga aliishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kufufua zao la
michikichi kwa kuwa linalenga kuinua uchumi wa Taifa.
Kikao
hicho kimehudhuriwa na Mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa, Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhadisi Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Ujenzi,
uchukuzi na Miundombinu, Mhandisi Atashasta Nditie, Naiubu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Jpsephat
Kandege, Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba.
Mpekuzi.
Comments