Waziri Kigwangalla Aagiza Ujenzi Wa Viwanda Vidogo Vya Asali Kwa Wilaya Zote Za Mikoa Ya Tabora Na Katavi.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ameuagiza Mfuko wa Ruzuku
wa Misitu Tanzania (TAFF) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) kuanzisha mradi wa viwanda vidogo vya kusindika na
kufungasha asali katika mikoa ya Tabora na Katavi ili kuongeza
uzalishaji wa zao hilo na kujenga uchumi wa viwanda.
Ametoa
agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mtakuja
wilaya ya Skonge mkoani humo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake mikoani
kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi na kutatua changamoto zake.
Alisema
kwa kiwango kikubwa wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa wategemezi kwenye
zao moja tu la tumbaku ambalo sio rafiki kwa mazingira kwakuwa miti
mingi hukatwa kwa ajili ya kukausha zao hilo jambo ambalo ni muhimu sasa
kuwekeza zaidi kwenye mazao mengine ikiwemo viwanda vya kusindika na
kufungasha asali ili kuongeza uzalishaji, ubora na hatimaye kuongeza
kipato na faida zaidi.
“Mwaka
huu ule mfuko wa misitu, kwa kiasi kikubwa tuamue tuwekeze ukanda huu
wa magharibi ambapo kuna zaidi ya asilimia 60 ya misitu yote hapa
nchini, na tuanze kwa kujenga kiwanda kimoja katika kila wilaya, ikiwemo
Nzega, Skonge, Uyui, Tanganyika, Mlele, Mpanda na Kaliua.
“Tuwawezeshe
wananchi wajiunge katika vikundi, tuwagawie mizinga ya kisasa, wafuge
nyuki kisasa, warine asali kisasa, wakisharina wapeleke kwenye viwanda,
ifungashwe kisasa, ipate bei kubwa, na mwisho wa siku wataona faida ya
kuwa na misitu.
“Hapo
tutakuwa tumewasaidia, watapa kipato mbadala lakini watakua wakali sana
kwa watu wanaoharibu misitu na tutatengeneza jeshi kubwa la wananchi la
ulinzi wa misitu yetu, hivyo nataka mradi huu uanze mara moja bila
kusuasua ili na sisi tuchangie jitihada za Serikali ya awamu ya tano
katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. ” alisema Dk. Kigwangalla.
Wakati
huo huo, Waziri Kigwangalla amewashauri wananchi wa mikoa hiyo
kuanzisha kilimo cha korosho kama zao jingine mbadala la kuongeza kipato
na kunusuru misitu badala ya kujikita kwenye zao moja la tumbaku ambalo
ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu ya mikoa hiyo.
Amesema
ni muhimu walau kwa kila kaya moja kuanza kwa kupanda ekari moja ya
mikorosho ili kuongeza zao jingine mbadala la biashara ambalo lina tija
zaidi kiuchumi na kiuhifadhi wa mazingira.
“Kilimo
cha tumbaku sio rafiki kwa mazingira tumejaribu kuleta mabani banifu
yanayotumia kuni chache, tumejaribu kuwashawishi wananchi wapande miti
lakini tumechemsha, miti mingi imeendelea kukatwa misitu nayo inateketea
siku hadi siku, ni lazima tutafute mbinu mbadala ya kukabiliana na
changamoto hii, na hii ni kupitia zao hili la korosho” alisema Dk.
Kigwangalla.
Amesema
tafiti zinaonyesha kuwa zao la korosho katika mikoa hiyo lina uwezo wa
kustawi zaidi na kuzalisha mara mbili kuliko mikoa ya kusini ambayo
inasifika zaidi kwa uzalishaji huo hapa nchini.
Aidha
ameziagiza halmashauri zote za mikoa hiyo kufanya utaratibu wa kupata
mbegu na miche ya zao hilo mapema iwezekanavyo kwa ajili ya kuwagawia
wananchi kabla ya msimu wa mvua kuanza na wataalamu wa kilimo
wawaelimishe wananchi njia bora ya kupanda na kutunza miche hiyo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Skonge, Peres Magiri alisema kiwango cha
mvua kwa mwaka katika wilaya hiyo kimeshuka na kufikia 600mm kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira.
Mpekuzi.
Comments