Kufuatia
Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwapangia jumla ya walimu 4,840 vituo vya kazi
kwenye Shule za Msingi na Sekondari nchini, Katibu Ofisi ya Rais, Tume
ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutaindurwa amewataka waajiriwa
hao kuzingatia kanuni na taratibu zinazosimamia utumishi wa walimu ili
kujiepusha na makosa ya kinidhamu.
Amesema
kuwa, kumekuwa na mazoea kwa walimu wengi kusaini nyaraka wanazopewa
wakati wa kuanza ajira bila kuzisoma kitu kinachosababisha kutoelewa
kanuni na taratibu za taaluma ya ualimu katika utumishi wa Umma.
“Wapo
walimu wengi ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na
wengine wamejikuta wakipoteza ajira zao kwa sababu ya kwenda kinyume na
Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu pamoja na zile
zinazoongoza Utumishi wa Umma” amesema Bibi Rutaindurwa.
Amefafanua
kuwa, Mwajiriwa atakaporipoti kwenye Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya
yenye Shule aliyopangiwa, atapewa mkataba wa ajira ulioandaliwa na Tume
ya Utumishi wa Walimu. Mwajiriwa anatakiwa kusoma mkataba huo pamoja na
viambatisho vyake ili aweze kujua haki na wajibu katika utumishi wake.
“Mara
nyingi walimu wanapoajiriwa, wengi wao wanasaini mikataba ya ajira
bila kuisoma na kuelewa. Sasa naelekeza kuwa, kila Mwalimu ahakikishe
anasoma mkataba wake na anauelewa vizuri kabla hajausaini ili kujua kwa
undani kile anachotakiwa kufanya katika utumishi wake” amesema Bibi
Rutaindurwa.
Ameongeza
kuwa, waajiriwa wanapaswa kusoma Sheria ya Utumishi wa Walimu ya mwaka
2015, Kanuni pamoja na Miongozo mingine ambayo inapatikana katika tovuti
ya Tume ya Utumishi wa Walimu kupitia www.tsc.go.tz.
Wakati
huo huo, Bibi Rutaindurwa amewataka Kaimu Katibu Wasaidizi Wilaya zote
kuhakikisha wanatoa ufafanuzi wa mikataba pamoja na kuwaelimisha walimu
walioajiriwa masuala mbalimbali yanayohusu ajira zao kwa mujibu wa
Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu na. 25 ya mwaka 2015.
Ameelekeza
kuwa, baada ya mwalimu kukamilisha taratibu zote za kiutumishi, Kaimu
Katibu Wasaidizi watoe barua za ajira kwa waajiriwa wapya kwa wakati
bila kuweka urasimu unaoleta usumbufu.
Ameongeza
kuwa, hatamvumila Mtendaji yeyote wa Tume ya Utumishi wa Walimu ambaye
atafanya uzembe au kuchelewesha barua za ajira kwa Walimu bila sababu
za msingi.
“Mwalimu
anapokamilisha kujaza nyaraka za ajira yake apewe barua ya ajira, bila
urasimu wowote ili aanze kutekeleza majukumu yake kwa haraka. Sitaki
kusikia mwalimu amechelewa kupata barua ya ajira au kuna mtumishi wa
Tume analeta urasimu kinyume na taratibu, kwa kweli sitamvumilia”
amesema Bibi Rutaindurwa.
Vilevile,
amewakumbusha Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuwashauri na kuwaelimisha
walimu juu ya kanuni na taratibu za kiutumishi badala ya kukaa na
kusubiri wafanye makosa ili wawachukulie hatua za kinidhamu.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015, Walimu
Wakuu na Wakuu wa Shule ndio mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa mwalimu.
Hivyo, walimu wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni za
Utumishi wa Walimu na zile za Utumishi wa Umma.
Adili Mhina,
Afisa Mawasiliano,
Tume ya Utumishi wa Walimu.
Mpekuzi.
Comments