Wahasibu
watatu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wamefikishwa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za uhujumu uchumi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 50 ya mwaka 2018 ni Mercy Semwenda (49) maarufu Mercy Frank Lema mkazi wa Mwananyamala, Frola Bwahawa (54) mkazi wa Mbagala na Hawa Tabuyanjaa (54) mkazi wa Mwenge.
Jana
Alhamisi Julai 12, 2018 wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita
alidai mbele ya hakimu mkazi, Augustine Rwizile kuwa washtakiwa
wanakabiliwa na mashtaka mawili ya wizi na kuisababishia hasara
Serikali ya Sh 57.7milioni.
Katika
shtaka la kwanza la wizi linalomkabili Mercy pekee anadaiwa katika
tarehe tofauti kati ya Januari Mosi, Septemba 21, 2017 jijini Dar es
Salaam, mshtakiwa aliiba vocha za muda wa maongozi zenye thamani ya
Sh44milioni.
Pia,
anadaiwa kuiba fedha za mauzo kiasi cha Sh5.9milioni na fedha taslimu
Sh 8.5milioni, vyote vikiwa na thamani ya Sh 57.7milioni mali ya TTCL,
wakati akijua kuwa ni mtumishi wa shirika hilo.
Katika
shtaka pili la kuisababishia Serikali hasara linalowakabili washtakiwa
wote, inadaiwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa
makusudi waliisababishia TTCL hasara ya Sh57.7milioni.
Baada
ya kusomewa mashtaka hayo, hakimu Rwezile alisema washtakiwa
hawatakiwi kusema chochote mahakamani hapo, kutokana na mashtaka
yanayowakabili kuwa ni ya uhujumu uchumi.
Hata hivyo, Mwita alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili
anayemtetea mshtakiwa wa pili na wa tatu, Thimotheo Wandiba alidai kuwa
wanafanya utaratibu wa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 24, 2018 itakapotajwa tena huku washtakiwa wakirejeshwa rumande.
Mpekuzi.
Comments