UNICEF, Madrasa Z’bar kuwaokoa watoto wasiosoma.

UELEWA mdogo juu ya umuhimu wa elimu walionao baadhi ya wazazi na walezi, ni miongoni mwa sababu zinazofanya watoto wengi kutokwenda skuli licha ya kutimiza umri wa kuandikishwa.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF visiwani Zanzibar, umebaini kuwa watoto wapaatao 140,000 wenye umri unaoanzia miaka 4-15, wapo nje ya skuli kwa sababu mbalimbali.

Sera ya elimu visiwani Zanzibar inawataka watoto wote kuanzia miaka minne hadi mitano kuandikishwa katika skuli za maandalizi, elimu ya msingi kuanzia miaka sita hadi 11, na sekondari miaka 12 hadi 15.

Akizungumza katika mkutano wa kutoa mafunzo ya kuandaa mkakati wa kuwarejesha skuli watoto walioko nje yanayofanyika katika kituo cha walimu wa maandalizi (MECP-Z) mjini Zanzibar, Meneja wa taaluma Sharifa Majid, ameyataja makundi matatu ya watoto wanaokosa masomo.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni ya watoto ambao hawajawahi kuhudhuria kabisa skuli, waliokwenda skuli na kutoroka (kwa muda wa miezi mitatu) na wale wasiohudhuria masomo mfululizo kwa mujibu wa utaratibu.

Meneja huyo alisema tafiti zinaonesha kuwa, wengi wa watoto walioko nje ya skuli ni kuanzia miaka 12-15, ambapo baadae wengine hulazimika kuanza masomo wakiwa na umri mkubwa.

Aidha alisema watoto wa kiume ndio wanaoongoza kwa idadi kubwa kuwa nje ya skuli ikilinganishwa na wanawake.

Zanzibarleo.

Comments