Tume
ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imeitaka Taasisi ya Twaweza
kujieleza ndani ya siku saba kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria kwa
kosa la kutoa matokeo ya utafiti bila ruhusa.
Barua hiyo ya Costech imesema, Twaweza waliomba kibali cha tafiti nne ambazo mmoja umekamilika na nyingine tatu bado zinaendelea.
Kwa
mujibu wa barua hiyo iliyosambaa mitandaoni ikionyesha imesainiwa na
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu, tume hiyo ndiyo yenye
mamlaka ya kusajili na kutoa kibali cha tafiti zote za muda mfupi na
mrefu zinazofanywa nchini.
Barua
hiyo imedai kuwa mwishoni mwa wiki, kulikuwa na taarifa za Twaweza
kutoa utafiti uliopewa jina la ‘Sauti za Wananchi’ ambao, tume haina
rekodi zilizoruhusu kuchapishwa kinyume cha sheria.
“Kwa
mujibu wa kifungu cha sheria namba 7 cha mwaka 1986, tume hiyo ndiyo
yenye mamlaka kusajili na kutoa kibali cha kufanyika tafiti nchini,”
imesema barua hiyo.
Taarifa kutoka Twaweza zinathibitisha taasisi hiyo kupokea barua kutoka Costech na kwamba wanaifanyia kazi.
Hivi karibuni Twaweza walitoa ripoti ya utafiti wa ‘Sauti za Wananchi’ ukielezea maoni ya wananchi kuhusu siasa nchini.
Utafiti
huo umeonyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa,
utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, Rais
anavyotekeleza majukumu yake tangu alipoingia madarakani na uhuru wa
kujieleza katika baadhi ya maeneo.
Mpekuzi.
Comments