Waziri
Mkuu mstaafu, Fedrick Sumaye, ameweka kile alichokieleza njama za
kufuta upinzani nchini na kutahadharisha kuwa kufanya hivyo ni kuondoa
sauti, uhuru wa watu na kwamba jambo hilo ni hatari kwa mustakabali wa
taifa.
Sumaye
ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, alieleza
hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa
marudio wa udiwani Kata ya Makorola jijini Tanga.
Alisema
kufuta upinzani ni kukataa demokrasia, hivyo kuwafanya watu wakose
mahali pa kusemea kero zao, jambo alilolifananisha na bomu ambalo alidai
linaweza kuleta madhara makubwa litakapo kuja kulipuka.
Aliwataka
Watanzania watambue kuwa kufutika upinzani nchini ni kusababisha
mapambano na kuondoa amani iliyopo kwa kuwa kushindana kwa vyama ndiyo
nguzo ya amani.
“Watanzania
msishabikie kuua upinzani maana yake mnashabikia kuua demokrasia na
kuondoa sauti za watu, maendeleo na uhuru wa watu kuongea matatizo yao,”
alisema Sumaye.
Alisema
sababu ya kufanyika chaguzi ndogo kila mara ni dalili za kukosekana kwa
demokrasia ya kweli na kwamba mabilioni ya fedha yanayotumika kwenye
uchaguzi huo yangetumika kuondoa kero mbalimbali za kijamii.
Alieleza
athari nyingine ya kuua upinzani ni kuzalisha vibaraka wengi na
kudumaza maendeleo na kuvishauri vyombo vya dola kutoingilia masuala ya
uchaguzi huo badala yake kazi hiyo iachwe kwenye ushindani wa vyama vya
siasa.
Alimwombea
kura mgombea wa kata hiyo anayeungwa mkono na Ukawa, Zainab Ashiraf,
ambaye alisema kumchagua kuwa diwani pamoja na mambo mengine, ni kukataa
ukandamizwaji wa demokrasia nchini.
Mkutano
huo uliofunguliwa na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Wilaya ya Tanga,
Richard Abel, ulihudhuriwa na vyama vinavyounda Ukawa ambao ni
mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe na Jonatha Bahweje
ambaye ni katibu wa Chadema Mkoa Tanga.
Wengine
waliohudhuria na kupewa nafasi ya kuzungumza ni Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi CUF, Amour Abal-hasan; Kamishna wa NCCR- Mageuzi, Ramadhan
Manyeko na Mbunge Viti Maalum Chadema, Yosephar Komba.
Mpekuzi.
Comments