Serikali Yatangaza Kiama kwa Wamiliki wa Leseni za Uchimbaji Madini na Vitalu Ambavyo Haviendelezwi.
Serikali
imetangaza kunyanganya leseni za uchimbaji madini ambazo hazitumiki kwa
muda mrefu pamoja na vitalu ambavyo vimehodhiwa na wachimbaji bila
kuendelezwa wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Pia imewataka wachimbaji wote wa madini ya dhahabu wanaofanya shughuli zao kwenye vyanzo vya maji na kuharibu mazingira kuondoka mara moja.
Makamu
wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo jana Jumatatu Julai 30
wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
Shule ya Msingi Chunya ikiwa ni siku yake ya siku kufanya ziara
kutembelea wilaya zote za Mkoa wa Mbeya.
“Ndugu
zangu tumesikia hapa kwamba kulikuwa na shughuli za uchimbaji madini
kwenye vyanzo vya maji na kama mnavyojua uchimbaji madini unatumia
madawa kadhaa ambayo wakisafisha yanaingia ndani ya mto.
“Sasa
vile vimelea vikiingia kwenye maji yale sio rahisi kusafishwa
vikaondolewa na Chunya vyanzo vya maji ni vichache na ndio maana
tumefunga migodi yote ambayo imekuwa ikifanya shughuli zake kwenye
vyanzo vile. Nasisitiza tena shughuli zozote zinazofanyika kule mtoni za
kuharibu maji, za kuharibu vyanzo vya maji zisimame mara moja na
waondoke, hatutawavumilia hawa watu,” alisema Samia.
Awali,
Waziri wa Madini, Angela Kairuki amesema kuna watu wamepewa leseni za
uchimbaji wa madini lakini hawaziendelezi wala vitalu walivyopewa pia
hawaviendelezi watazinyang’anya leseni hizo na kuwapatia wengine wenye
uhajitaji.
Alisema
hilo linakuja baada ya malalamiko ya wachimbaji wadogo ambao hawana
maeneo ya kuchimba madini lakini maeneo makubwa yamehidhiwa na
wachimbaji wakubwa ambao hawayaendelezi.
“Mheshimiwa
Makamu wa Rais, wapo watu wamepewa leseni za uchimbaji madini lakini
lakini hawazitumii leseni hizo, hawajaendeleza maeneo ya uchimbaji
ambayo wamepewa na kwa kuwa wilaya hii (Chunya) imejikita zaidi kwenye
uchimbaji madini niseme katika hadhara hii tunawapa onyo la mwisho wale
wote tuliowapa leseni lakini hawaziendelezi tutazifuta na kuwapa watu
wengine wenye nia ya kuwekeza.”
Mpekuzi.
Comments