Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesimulia namna viongozi wa Mkoa wa
Songwe walivyomdanganya na kufanya ujanja ili asitembelee Wilaya ya
Songwe kwa kisingizio cha ubovu wa barabara.
Akizungumza
kwenye majumuisho ya ziara yake ya siku tano, Makamu wa Rais alisema
viongozi hao walimdanganya kuwa wilaya hiyo iko mbali na barabara na
haipitiki kirahisi.
Alisema
viongozi hao akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa, walimzuia
kutembelea wilaya hiyo kwa kuwa walikuwa wakijua hakuna mradi wa
kuzindua, lakini wakasingizia ubovu wa barabara.
Alisema,
aliambiwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuwa wilaya hiyo ina barabara mbovu
na ni mbali, lakini baada ya uchunguzi alioufanya kupitia vyombo vyake,
aligundua sababu ya kutopelekwa huko ni kukosekana kwa mradi wa
kuzindua.
Aliongeza
kuwa wilaya hiyo ni tajiri ina fursa za uchimbaji wa madini ya dhahabu
hivyo kutokuwa na mradi ni udhaifu wa viongozi wa halmashauri na
kuwataka wajitathmini kwa kuwa wanaonekana hawajui wajibu wao.
''Aliniambia
Mkuu wa Mkoa kuwa Songwe ni mbali na barabara ni mbovu…ni sawa, lakini
vyombo vyangu vimebaini kuwa sababu kubwa ni kwamba hakuna mradi wa
kuuzindua viongozi mjitathmini,'' alisema Samia.
Katika
hatua nyingine, Samia aliwasihi wananchi wa Songwe hasa Halmashauri ya
Tunduma kuzaa kwa mpango ili waweze kumudu gharama za masomo.
Samia
alimaliza jana ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Songwe kwa
kutembelea vituo vya afya, mradi wa maji, shamba la miti pamoja na
kuzungumza na watumishi kupitia vikao na wananchi kupitia mikutano.
Mpekuzi.
Comments