JWTZ Yawatoa Hofu Wananchi Baada ya Magari yao ya Kijeshi Kuonekana Yakizunguka Ukuta wa Madini ya Tanzanite.
Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limefafanua sababu za kuonekana magari
ya dereya eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite, Mirerani wilayani
Simanjiro mkoani Manyara.
Msemaji
wa JWTZ, Kanali Ramadhani Dogoli aliliambia gazeti la Mwananchi jana
kuwa magari hayo yalikuwa yakitengeneza njia kwa ajili ya doria
kuzunguka ukuta uliojengwa katika eneo la migodi ya machimbo hayo.
“Hakuna
operesheni inayofanyika kama inavyodhaniwa na watu, tunachokifanya ni
kutengeneza njia kuzunguka mgodi ili iwe rahisi kufanya doria,” alisema.
Kanali Dogoli alisema vinavyoonekana si vifaru vya kivita, bali ni magari maalumu ya doria za kijeshi na hasa porini.
“Jeshi
haliwezi kupeleka vifaru maeneo yenye makazi ya watu, vifaru vinatumika
kwenye vita pekee, yaliyoonekana kitaalamu tunayaita magari ya deraya,”
alisema msemaji huyo.
Kanali
Dogoli aliongeza kuwa, “ukuta ule ni mrefu na hatuwezi kufanya doria
kwa miguu, hivyo ni lazima tutatumia magari ambayo ni maalumu kwa njia
za porini, si vifaru vile.”
Kuonekana kwa magari hayo kulizua taharuki baadhi ya wananchi wakisema ni vifaru.
Mkuu
wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aliwatoa hofu wakazi wa
Mirerani baada ya kuonekana magari hayo kuwa wao ni raia wema, hivyo
hawapaswi kuogopa.
Alisema wanajeshi kazi yao ni kulinda nchi na wanatambua namna ya kulinda, hivyo hawapangiwi.
Chaula
alisema wanaimarisha ulinzi nje ya ukuta na pia kuweka mazingira safi
ili mtu yeyote akipita aonekane. Aliongeza kuwa, kila baada ya mita 100
kutakuwa na kibanda cha mlinzi atakayelinda ndani na nje ya ukuta.
Alisema ulinzi unaimarishwa kwa kuwa wananchi wengi wanafanya mambo kwa mazoea badala ya kufuata sheria, kanuni na utaratibu.
Mpekuzi.
Comments