Balozi Seif alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na uongozi wa
wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ulioongozwa
na naibu Waziri wa wizara hiyo, DK. Suzan Alphonce Kolimba, aliyefika
ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema viongozi hao wa wizara wanapokutana inasaidia
kubadilishana uzoefu wa kiutendaji hali ambayo husaidia kuimarisha
jukumu la msingi la kuwahudumia vyema wananchi.
Alisema hatua ya kukutana kwa mawaziri wa wizara zinazofanana baina
ya serikali zote mbili ni muhimu na ilikuwa ikifanyika katika vipindi
tofauti hali ambayo itaendelea kujenga umoja na mshikamano baina ya
watumishi wa serikali zote mbili.
Alisema mikutano na vikao vya mara kwa mara vya mazungumzo
vinavyowajumuisha mawaziri wa wizara zinazofanana za pande hizo mbili
hasa pale zinapojichomoza hitilafu ndogo ndogo katika pande mbili za
muungano husaidia kupunguza kero za muungano.
“Vikao vya mara kwa mara vya mawaziri wa wizara zinazofanana baina ya
SMZ na SMT vina uwezo wa kupunguza au kuondoa kabisa vile vikao vya
watendaji Wakuu wanaokutana kujadili kero zilizopo kwenye muungano”,
alisema.
Akitoa shukrani kwa niaba ya uongozi wa wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Kolimba alisema kazi inayokabili
viongozi hasa mawaziri wapya ni kuendelea kupata mawazo na fikra za
watangulizi wao ili jukumu walilokabidhiwa walitekeleze kwa ufanisi
uliotukuka.
Dk. Kolimba alisema licha ya taaluma waliyokuwa nayo viongozi
wachanga lakini bado busara na hekima za wale wazoefu zinapaswa
kujumishwa pamoja katika utendaji wao kwa lengo la kuwatumikia vyema
wananchi wengi mjini na vijijini Tanzania bara na Zanzibar kwa ujumla.
Zanzibarleo.
Comments