Balozi Seif afungua tamasha la mzanzibari.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema kuwa kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji kwa watoto wadogo, pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya, ni dalili tosha inayoashiria kumong’onyoka kwa utamaduni.

Alisema kuwa ili kujiepusha na tishio hilo, serikali imeanzisha tamasha la Mzanzibari ambalo pamoja na mambo mengine, ni chombo cha kuulinda na kuuendeleza utamaduni huo kwa kukumbusha na kurejesha jamii wapi inatoka.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akifungua rasmi tamasha la 23 za utamaduni wa Mzanzibari, kwenye viwanja vya Mapinduzi Square Kisonge, ambapo hutuba yake ilisomwa kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo.

Alisema kuwa jamii yenye kubeza utamaduni wake hutumbukia kwenye shimo la mtafaruki,  jamii hiyo hukosa utambulisho ambao ni sawa na bidhaa inayouzika  sokoni kwa bei ya juu kabisa, na kama mipango madhubuti itaandaliwa  jamii inaweza kustawishwa kwa kutumia utamaduni wa Kizanzibari.

Alisema kuwa ustarabu wa Zanzibar ni matokeo ya utamduni ambao umeijengea sifa kubwa tangu zama za kale, na historia mbali mbali imeandikwa juu ya jambo hili, ambapo watu kutoka mataifa ya Ulaya, Asia na hata Afrika hutembelea Zanzibar na wengine kuamua kufanya maskani yao.

Zanzibarleo.

Comments