Zitto Kabwe Ajitosa Kuwapigania Wakulima wa Korosho Kwa Kupinga Marekebisho ya Sheria Mpya ya Zao Hilo.
Mbunge
wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema chama hicho
kitashirikikiana na wabunge wa vyama vya upinzani kupinga marekebisho ya
Sheria ya Sekta ya Korosho namba 203.
Jana
Jumatano Juni 20, 2018, Zitto ametoa taarifa katika mitandao mbalimbali
ya kijamii akipinga mabadiliko hayo, kutaka wananchi kukataa kile
alichokiita dhuluma kwa wakulima wa korosho.
Zitto ametoa kauli hiyo wakati Serikali ikikusudia kuifanyia marekebisho sheria hiyo.
Kwa
mujibu wa muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2018, inapendekezwa
kufutwa mgawo wa fedha zinazotokana na ushuru wa kusafirisha korosho nje
zilizokuwa zikitolewa kwa wakulima ili kuboresha zao hilo.
Badala yake, muswada unapendekeza fedha hizo kupelekwa mfuko mkuu wa Hazina kama fedha nyingine za Serikali.
Sheria
ya sasa inataka asilimia 65 ya fedha zinazotokana na ushuru wa
kusafirisha korosho nje kupelekwa kwa wakulima kupitia Bodi ya Korosho
(CBT).
"Sisi
ACT Wazalendo, kwa kushirikiana na wabunge wote wa upinzani, pamoja na
wale wa CCM watakaokuwa tayari kuwatetea, tutajitahidi sana kuhakikisha
mapendekezo haya hayapiti,” amesema Zitto katika taarifa yake hiyo,
akiwaeleza wananchi kuhusu mabadiliko hayo.
"Lakini Kuna haja kubwa ya wananchi, wakulima wa korosho, hasa wa mikoa ya kusini, kupaza sauti kukataa. Tusikubali.”
Amesema
katika marekebisho hayo Serikali inapendekeza kufuta mgao wa fedha
zinazotokana na ushuru wa kusafirisha korosho nje, “katika mgao wa sasa
wa fedha hizo Serikali huchukua asilimia35 ya fedha, na asilimia 65
inayobakia hupelekwa kwenye mfuko wa kuendeleza zao la korosho nchini.”
“Fedha
hizo kuingizwa mfuko mkuu wa Hazina kama fedha nyingine za Serikali, na
hivyo kutumika kwa asilimia 100 kwa mambo mengine na sio kwaajili ya
kuendeleza zao la korosho.”
Amedai
Serikali imegoma kutoa asilimia 65 ya uendelezaji korosho na
imeshazitumia fedha za Korosho Sh211bilioni kinyume cha sheria ya sasa.
“Wameamua
sasa kufuta hiyo sheria ya korosho kabisa ili wasibugudhiwe.
Tutapambana bungeni kupinga dhuluma hii dhidi yenu, ikishindikana
tutarudi kwenu,” amesema.
Mpekuzi.
Comments