Zanzibar yajivunia mchango wa UNICEF.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imelihakikishia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) kuwa litaendelea kuthamini mchango wa shirika hilo katika kuhakikisha watoto wa Zanzibar wanaendelea kupata haki zao za msingi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Ussi Haji Gavu, aliyasema hayo katika hoteli ya Park Hyyat, Shangani mjini Zanzibar wakati wa hafla fupi iliyotayarishwa na Ofisi ya Rais kwa ajili ya kumuaga Ofisa Mkuu wa UNICEF Zanzibar, Francesca Morandini, aliyemaliza muda wake wa kazi Zanzibar.
Alisema serikali inathamini ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na shirika hilo huko akitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Ofisa Mkuu huyo kwa ushirikiano wake katika kipindi chote alichofanya kazi Zanzibar.
Alieleza kuwa katika muda wake wote wa kazi, alitoa ushirikiano mzuri kwa wizara na taasisi za serikali jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliokusudiwa.
Nae Francesca,  alitoa shukurani na pongezi kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kumuandalia hafla hiyo fupi ya kumuaga na kueleza kuwa tukio hilo limeonesha wazi kuwa serikali inavyothamini juhudi za shirika hilo.
Zanzbarleo.

Comments