
Akizungumza na Waandishi wa habari Waziri wa Wizara hiyo Balozi Amina Salum Ali amesema Mfumo huo wa usajili kwa kutumia mtandao ni miongoni mwa matokeo ya jitihada za serikali ya mapinduzi zanzibar za kuhakikisha taratibu za uanzishaji na uendeshaji wa biashara unaimarishwa zanzibar ambapo hatua hiyo itarahisisha urasimishaji na uendelezaji wa biashara pamoja kuwapunguzia gharama wafanyabiashara ili kuwavutia wawekezaji zanzibar.
Amesema pia mfumo huo mpya wa usajili unafaida mbalimbali ambapo miongoni mwa faida hizo ni kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu na upatikanaji wa taarifa za wateja pindi wanapohitajika,pia kuweka mazingira bora ya biashara na kuendana na vigezo na mifumo ya kimataifa.
Hata hivyo utasaidia kuondoa usumbufu na kurahisisha upatikanaji wa huduma za usajili kwa urahisi pamoja na kuongeza na kuimarisha mashirikiano ya kikazi baina ya wakala wa usajili biashara na mali zanzibar na taasisi nyengineza serikali na binafsi.
Aidha Balozi Amina amesema mfumo huo ni misingi wa kuimarisha mashirikiano miongoni mwa taasisi za kodi pamoja na taasisi nyengine zinazohusika na uanzishaji na uendelezaji wa biashara kwa kuweka kituo kimoja cha usajili wa biashara.
Kwaupande wake Msaidizi Mrajis wa Makampuni Makubwa ya Kibiashara zanzibar AbdulBaq Khabib Ali amesema mfumo huo utawasaidia zaidi wafanyabiashara wote wakubwa na wadogo katika kusajili biashara zao na utaweza kuondoa migogoro mbalimbali inayokwamisha biashara zao.
Aidha AbdulBaq amewataka wafanyabiashara kutoa mashirikiano mazuri katika matumizi ya mfumo huo ili kurahisisha upatikanaji ya maendeleo katika biashara zao na endepo mfanyabiashara atakaidi agizo la usaji wa biashara zao kwa mfumo huo wa kimtandao biashara hizo hazitofahamika kisheria pia watafungiwa kuuuza kwani watakuwa wanafanya makosa kisheria.
Amesema ili wafanyabiashara waende sambamba na serikali basi ni wajibu wao kutumia mfumo huo kusajili biashara zao kwani mfumo huo umeweza kuunganisha taasisi zote za kodi kuweka kituo kimoja cha usajili wa biashara.
Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr.Ali Mohamed Shein siku ya Jumatatu katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakili.
Zanzibar24.
Comments