Wastaafu 164 polisi walia ugumu wa maisha wakisotea mafao.

Msemaji wa jeshi la polisi nchini, BarnabasWastaafu 164 wa Jeshi la Polisi wanasotea mafao ya kiinua mgongo kwa takriban mwaka mmoja sasa, wakiutaja ugumu wa maisha kuanza kuwaumiza taratibu.
Tangu Julai 2017, wastaafu hao wamekuwa wakisubiri mafao yao.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa amesema suala hilo linashughulikiwa na hundi za malipo zinaendelea kutolewa kwa kadri zinavyokamilika.
Mwakalukwa alisema polisi wana utaratibu wa kuwaandaa wastaafu kwa kuwapa elimu, ikiwamo kujaza fomu na kufanya ufuatiliaji kwenye kitengo cha mafao ndani ya jeshi hilo.
Alisema kuna pande mbili zinapaswa kufuatilia ili kulipwa.
Mafao wanayodai ni kutoka mfuko wa Pensheni wa PSPF.
Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki, Mwakalukwa alisema wastaafu wa mwaka jana wako 189 na kati yao, 25 wameshalipwa hivyo waliosalia ni 164 na kwamba, wanatarajia kuanzia wiki hii kuna hundi zitatolewa kwa ajili ya wastaafu hao.
Mwakalukwa alisema ucheleweshaji unaweza kuwa umechangiwa na mambo mengi ikiwamo kutokamilika kwa nyaraka muhimu za malipo zinazowahusu mwajiri na mwajiriwa.
“Ingekuwa hawamo kwenye orodha ya malipo lingekuwa ni tatizo lingine, hawa lazima walipwe, wamo kwenye orodha na wenzao wameshalipwa,” alisema. Mwakalukwa alisema mfumo wa malipo ya kiinua mgongo uliopo ni mzuri, isipokuwa kunaweza kujitokeza usumbufu kwa mtu mmojammoja kwa sababu ya kushindwa kukamilika kwa nyaraka.
Mmoja wa wastaafu hao, Julius Hizza alilieleza Mwananchi kuwa kuchelewa kwa mafao yao kumechangia ugumu wa maisha. “Nilijiunga na Jeshi la Polisi tangu mwaka 1982, namba yangu ni D9477, tumezunguka kwa muda mrefu mimi na wenzangu tuliostaafu pamoja, hizi kauli za njoo kesho, njoo mwezi ujao zimetuchosha,” alisema Hizza.
Hizza alisema anazitegemea fedha za mafao zimsaidie katika mambo mengine ikiwamo kulipia ada za watoto.
Ofisa uhusiano mwandamizi wa PSPF, Abdul Njaidi alisema si mafao ya polisi pekee wanayoyashughulikia, bali zipo pia taasisi zingine.
“Kazi ya mfuko ni kulipa mafao na kuhudumia wastaafu ambayo tunaifanya vizuri kama utaratibu unavyotaka, ikitokea kuchelewa ni matatizo ya mtu binafsi ambayo pia tunashiriki kuhakikisha ufumbuzi unapatikana,” alisema Njaidi.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni hivi karibu, waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alizungumzia mafao na mirathi katika mwaka wa fedha wa 2017/18 akisema Serikali ilitenga Sh1.6 trilioni kwa ajili ya kulipia michango ya mifuko ya hifadhi za jamii.
“Hadi kufikia Aprili, Sh716.19 bilioni sawa na asilimia 71 zilitumika kulipa michango ya mwajiri kwa watumishi wa umma,” alisema.

Comments