Wabunge CCM wagawanyika.

Wabunge wa CCM wamegawanyika bungeni kutokana na hoja kuhusu mabilioni ya wakulima yanayotokana na asilimia 65 za ushuru wa mauzo ya nje ya korosho na mabadiliko ya sheria kuhusu ushuru huo.
Kutokana na mjadala mkali kuhusu suala hilo, mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), aliwatahadharisha wabunge wa chama hicho wanaokikosoa ndani ya Bunge.
Wakati Lusinde maarufu Kibajaji akisema hayo, katibu wa wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza alisema ndiye anayepanga orodha ya wachangiaji wa chama hicho na si Serikali, akimjibu mbunge mwenzake Hawa Ghasia.
Hayo yalijitokeza bungeni jijini Dodoma jana ikiwa ni siku ya mwisho kwa wabunge kuijadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19.
Leo Serikali itajibu hoja zilizoibuliwa na kisha wabunge watapiga kura kupitisha au kuipinga bajeti hiyo ya zaidi ya Sh32 trilioni.
Hali ilivyokuwa
Wakichangia mjadala wa bajeti wabunge wa CCM, Nape Nnauye (Mtama) na Ghasia (Mtwara Vijijini) walisema kinachofanywa na Serikali kinakwenda kukiua chama hicho katika mikoa ya kusini.
Wabunge hao waliowahi kuwa mawaziri walisema wako tayari kudhalilishwa na wabunge wenzao waliopangwa kuitetea Serikali katika sakata la korosho.
Nape alisema korosho kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani na mingine 17 iliyoongezeka kulima zao hilo ni maisha ya wananchi.
Alisema kama wakulima wa pamba wakizungumzia zao hilo wanazungumza maisha, wao hawana mifugo wala almasi.
“Tukizungumza korosho ni maisha na linapozunguzwa hili ushabiki uwekwe pembeni, tunazungumza maisha ya watu. Wengi wanapotosha na wanaopotosha hawalimi korosho na wanaopotosha hawapigiwi kura na wakulima wa korosho na sisi lazima tuiambie Serikali ukweli,” alisema Nape.
Alisema ushuru huo ulipoanza walikusanya Sh800 milioni, lakini zilipofika zaidi ya Sh100 bilioni kelele zikaanza.
Alisema kuna dhana inajengeka kuwa mapato yote ya korosho yasaidie kusini ambayo si kweli.
“Wanaosema si hela zetu, hiki kiatu hamvai ninyi, tunakivaa siye, Dk Mpango (Philip-Waziri wa Fedha) kuweni na huruma na mapendekezo haya yanakwenda kuiua CCM kusini, yanakwenda kutuweka mahali pagumu sana,” alisema Nape.
Baada ya kauli hiyo, naibu waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alitoa taarifa akisema Nape asipende kila wakati anapochangia kuwafanya wananchi wa kusini kupinga jambo, kwamba kusini wataenguliwa kwa korosho.
Nape aliikataa taarifa hiyo akisema, “Niwaombe wananchi wanakolima korosho, wamsamehe mama yangu na shangazi, hajui analolisema. Tunazo takwimu mama yangu hajui. Majimbo tuliyokosa kusini kwa jinsi tulivyoshughulikia suala la gesi.”
“Wako wabunge wamechomewa nyumba zao, tunaposema hapa tunatahadharisha, nimetoka kule juzi hali mbaya, kama tunataka kuziba masikio tunaweza kutumia ubabe kupitisha, kuamua uzima au mauti na yote yako mbele, kupanga ni kuchagua, kazi yetu ni kutahadharisha na karibuni kusini mtayaona.”
Nape aliungwa mkono na Ghasia ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti aliyesema, “Kwa masikitiko kuna wabunge wamekaa vikao, wameandaliwa waje kutudhalilisha wabunge tunaowatetea wakulima.
“Wabunge wote tuna haki sawa za kutetea wananchi wetu, anayetoka katika pamba atetee pamba, anayetoka katika madini atatetea madini yake na anayetoka katika korosho atatetea wa korosho.
“Niwahakikishie wakulima wanaolima korosho wabunge wao tutapambana hata haki isipopatikana ila tutawatetea. Tunaambiwa sisi wabinafsi, korosho inalimwa kwa kiwango kikubwa na mikoa miwili au mitatu lakini tulipokaa katika kamati tukakubaliana na kwenda mikoa 17.”
Ghasia alisema: “Mimi utafiti wangu wa shahada ya kwanza na ya pili unahusu korosho. Leo mtu anakuja humu anaijua korosho na ninasema kila mtu atetee lake na wananchi mjiandae kuwasikia.
“Tudhalilisheni, tuchambeni ila bado tutaisema korosho. Mimi nilikaa upande wa kutetea gesi lakini nilichomewa moto nyumba, mikorosho ya baba yangu ilikatwa, mabomba ya maji yaling’olewa na katika hili nilimpoteza baba yangu, siko tayari kuchomewa moto, siko tayari.
“Wale wenye nia njema waendelee kuwa na nia njema na wale wenye nia ovu wadhihirishe hapahapa duniani.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge), Jenista Mhagama aliomba mwongozo akisema, “Hili jambo ambalo tunaliona tukiliacha si sahihi sana na hasa Serikali inapotuhumiwa kwamba ina nia ovu ya kuwanyanyasa au kuwadhulumu wananchi wa Tanzania wanaotoka mikoa ya kusini na hasa hili jambo la korosho.”
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu alisema mjadala usiwe kitu cha kuligawa Bunge na kwamba, wabunge wana uhuru wa kujadili kwa utaratibu wa kibunge uliowekwa na Serikali ina majibu mazuri ya kujibu hoja za wabunge.
Wabunge wengine walioungana na akina Nape na Ghasia katika suala la korosho ni Willy Qambalo (Karatu-Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi), James Ole Millya (Simanjiro-Chadema) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki-Chadema).
Rweikiza awajibu
Akichangia bajeti, Rweikiza alisema ndiye anayepanga orodha ya wachangiaji na si Serikali.
“Mimi ndio napanga wa kuchangia si Serikali kauli ya Ghasia kuwa kuna watu wamepangwa na Serikali kutetea hoja hiyo si ya kweli. Hata Ghasia hakuwa katika orodha ya wachangiaji lakini nimempanga,” alisema Rweikiza ambaye ni mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM).
Rweikiza alisema mjadala wa fedha za ushuru wa mauzo ya korosho nje ni kutofautiana uelewa, lakini Serikali iliweka ushuru huo kwa lengo la kuzuia mazao ghafi kupelekwa nje jambo ambalo lipo katika mazao mengine ya kahawa, katani, tumbaku na mengine.
Baadhi ya wabunge walianza kupiga kelele wakipingana na kauli hiyo jambo lililosababisha Zungu kuwataka wabunge kutulia ili kumpa nafasi mbunge huyo kuchangia.
Kauli hiyo ilimfanya, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe kusimama kutoa taarifa kuwa mbunge huyo analipotosha Bunge kwa sababu ushuru huo ni fedha za wakulima.
Rweikiza aliikataa taarifa hiyo akisema inatokana na uelewa wa mbunge husika lakini si sawa kutoa fedha hizo kwa wakulima wa korosho na kuwaacha wakulima wengine.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Jacqueline Ngonyani aliunga mkono hoja ya Serikali ya kuchukua asilimia zote 100 za ushuru huo.
Kauli hiyo ilimfanya mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu Bwege kusimama kumpa taarifa akisema kabla ya kupelekwa mfuko mkuu wa Hazina wapate kwanza fedha za korosho.
Onyo la Lusinde
Mbunge wa Mtera (CCM), Lusinde alisema, “Humu ndani tunapochangia tujiepushe na kazi za wengine. Eti tukifanya hivi tutashindwa, sisi si wasemaji wa chama.”
“Sisi wabunge wa CCM kazi yetu ni kuisimamia Serikali, kuikosoa na kuitetea na nasema kama bosi wenu humu ndani. Natoa marufuku kwa mbunge wa CCM kukizungumzia chama humu.”
Lusinde alisema, “Hiki ni chama chenye Serikali, kuisimamia si kukikosoa chama. Kuweza sisi kushinda au kushindwa si sehemu yake. Kama wabunge wangu hamna lugha ya kumsifia Rais au kukosoa tulieni.”
Kuhusu korosho alisema, “Maneno mengi yamesemwa na bora yakasemwa kwani hili ni jumba la kusema hayo maneno.”
Aliwaomba wanasheria waliopo bungeni kutoa ufafanuzi unaoeleweka juu ya suala la ushuru wa mauzo ya bidhaa nje.
Kutokana na kelele za mara kwa mara kuibuka, Bwege alijikuta akitolewa ndani ya ukumbi wa Bunge na mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Ahmadi.
Mwananchi.

Comments