
Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Mohammed Aboud Mohammed ameyasema hayo leo Juni 26,2018 wakati akitoa hotuba Kwa wananchi katika maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya duniani ambapo kwa Zanzibar yalifanyika katika viwanja vya Mapinduzi square,
Mhe. Mohammed Aboud amesema serikali ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania itaendelea kusimamia mikakati na mipango madhubuti iliyopangwa ya kuwakomesha wale wote wanaojihusisha na uingizaji usambazaji na uzaji wa dawa za kulevya nchini.
“Tutawashughulikia ipasavyo wale wote ambao wanajihusisha na vitendo hivi na hapa hatutaangalia nafasi ya mtu, cheo alichokuwa nacho, awe mwanachama mwenzetu au watoto wetu tukiwabaini tutawashughulikia ipasavyo” alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Mohammed Aboud Mohammed.
Pia alisema serikali zote mbili zitaendelea na jitihada ya kuhakikisha wanalinda na kuhifadhi mila na utamaduni wa Watanzania kwa kuweka misingi iliyobora ambayo itawaepusha na utumiaji wa dawa za kulevya ambayo hupelekea kuongezeka kwa vitendo viovu kama wizi na ukabaji na hata vitendo vya udhalilishaji.
Aidha Mhe. Aboud amewataka wanajamii kuacha tabia ya kuwanyanyapaa na kuwatenga wale vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya, wawape moyo na kuwanao karibu katika shughuli za kijamii ili kuepusha uwezekano wa kurudi tena katika athari na matumizi ya dawa za kulevya.
Nae Afisa wa Jeshi la polisi kitengo kinachoshughulika na udhibiti wa dawa za kulevya Hamisi Juma Ame amesema uwepo wa bandari bubu nyingi katika visiwa vya Zanzibar ni moja ya changamoto ambayo inawakabili na kupeleke kurudisha nyuma jitihada zao za kupambana na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.
Pia amewataka wadau mbalimbali nchini kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja kuwapatia mbinu ambazo zimekuwa zikiibuliwa kila siku na waingizaji pamoja na wasambazaji wa dawa za kulevya nchini.
Maadhimisho hayo ya kupiga vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya duniani huadhimishwa kila ifikapo juni 26 ya kila mwaka ambapo kaulimbiu ya mwaka huu “TUENDELEZE MAISHA YETU, JAMII YETU NA UTAMBULISHO WETU, BILA YADAWA ZA KULEVYA”.
Zanzibar24.
Comments