Ilikuwa hivi. Baada ya kipindi cha maswali na majibu leo Juni 26, Spika kama kawaida alianza kutambulisha wageni. Lakini leo hakuanza moja kwa moja, bali alianzia mbali huku akimwaga sifa kem kem wakati huo wabunge wakiwa hawajui Spika Job Ndugai anataka kutoa tangazo gani.
“Hivi karibuni mlisikia kupitia vyombo vya habari kuwa ndugu Jivunie Mbunda alikuwa amefunga ndoa na hapa leo wamekuja kulitembelea Bunge,” amesema Spika Ndugai.
Mara baada ya kumaliza kumtaja na kumuomba yeye na mkewe wasimame, mke alisimama na kumbeba mumewe wakiwa na mavazi nadhifu huku Bunge likilipuka kwa furaha.
Jivunie Mbunda ni mlemavu mwenye kimo kifupi ambaye alifunga ndoa na Bahati Ramadhani Mei 12 mwaka huu, Liwale, Lindi.
Bahati alitumia kama dakika moja hivi akiwa amembeba mumewe Mbunda kifuani, huku Mbunda akionyesha tabasamu.
Wakati tukio hilo likiendelea, wabunge waliimba ‘bebi, bebi, bebi na makofi na vigelegele vingi vilisikika kutoka kwa wabunge na kufanya Bunge lisimame kwa dakika mbili nzima.
Baada ya hayo, Spika akasema leo saa saba wageni hao ambao walipelekwa bungeni na Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka, wasitoke hadi wafike ofisini kwa Spika ili wazungumze.
Wabunge wamekubaliana kukatwa Sh20,000 kwa kila mbunge kwa posho za leo ili kuwachangia maharusi hawa.
Uamuzi huo umefikiwa na kuungwa mkono na wabunge baada ya Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea kutoa hoja ya kuwachangia.
“Kwa kuwa kwa kawaida maharusi wanapotaka kufunga ndoa huomba michango, lakini maharusi hawa hatukupata fursa ya kuwachangia, naomba kutoa hoja ya kukatwa posho yetu ya leo ya Sh20,000,” amesema Mtolea.
Baada ya kauli hiyo, Spika Ndugai aliwahoji wabunge na wengi waliafiki hoja hiyo.
Mwanchi.
Comments