Mbunge
wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ anaweza kufikishwa
mahakamani kwa kushindwa kurejesha mkopo wa Benki ya Taifa ya Biashara
(NBC), tangu mwaka 2007.
Kwa
kushindwa kurejesha mkopo huo ambao pamoja na riba umefikia Sh784.5
milioni, benki hiyo imemwandikia barua mdhamini wake, Martin Nandi
ikimjulisha hatua itakazochukua dhidi ya nyumba yake ndani ya siku 60.
Nyumba hiyo iliyoko kiwanja namba 275, kitalu H, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ndiyo ilitumika kama dhamana ya mkopo huo NBC.
Katika
barua ya Machi 21, benki inamtaarifu mdhamini huyo kuwa ndani ya siku
60 inaweza kuipiga mnada mali hiyo ya dhamana, kuiweka chini ya mfilisi,
kuipangisha au kuiweka chini ya umiliki wake benki.
Nandi
baada ya kupata barua ya NBC, kupitia kampuni ya uwakili ya Raymaxx
Attorneys, amemwandikia Musukuma taarifa ya kusudio la kumfikisha
mahakamani.
Katika
taarifa iliyosainiwa Aprili 20 na wakili Rabin Mafuru, Nandi alimpa
Musukuma siku saba za kulipa deni la NBC na pia amrejeshee hati ya
nyumba yake.
Musukuma alipoulizwa kuhusu barua hiyo hakuwa tayari kuizungumzia akisema tayari kuna kesi mahakamani.
“Kuna
kesi mahakamani sasa mimi nitazungumza kitu gani. Hilo suala liko
Mahakama Kuu na yeye amefungua kesi sasa mimi nitazungumza kitu gani?”
alisema Musukuma.
Alisema, “Kama unataka kuandika alivyotaka yeye mimi sijui lakini mimi siwezi kuzungumza kitu chochote kilichoko mahakamani.”
Kwa
mujibu wa Nandi na nyaraka kuhusu mkopo huo , Juni 16, 2007 aliingia
mkataba wa makubaliano ya ubia katika biashara ya simu na Musukuma.
Anadai
waliingia mkataba baada ya Musukuma kumuomba ampatie hati ya nyumba
yake kwa ajili ya kuchukua mkopo NBC ili kuendeleza biashara hiyo.
Kwa mujibu wa barua ya Juni 16, 2007 Musukuma alikiri kupokea kutoka kwa Nandi hati ya nyumba kwa ajili ya mkopo kutoka NBC.
Nandi alisema hati hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya mkopo wa Sh65 milioni lakini iliendelea kutumika kwa mikopo mingine.
Anadai
masharti ya dhamana yalikuwa Nandi kuwa mkurugenzi katika kampuni ya
Musukuma ya simu za mkononi baada ya mkopo kutolewa na benki.
Masharti
mengine yalikuwa wote wawili kuwa watia saini katika akaunti maalumu ya
mkopo huo, kufanya tathmini ya faida halisi ya mauzo kila mwisho wa
mwezi na kugawana faida kwa kiwango cha asilimia hamsini kwa hamsini.
Mengine
ni kuhuisha mkataba wa mkopo huo kila ifikapo Desemba 31, iwapo wote
wataridhika na ustawi wa biashara na faida kwa kuzingatia masharti
waliyowekeana. Nandi anadai baada ya mkopo kupatikana, Musukuma
alimkwepa na kukataa kusainiana mkataba wa kisheria kulingana na
makubaliano yao.
Chanzo: Mwananchi na Mpekuzi.
Comments