Mchango wa Mchungaji Msigwa bungeni Dodoma wageuka gumzo Kenya.

Mchungaji Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), wiki iliyopita aligeuka gumzo ‘kiaina’ nchini Kenya.
Video inayomuonyesha mbunge huyo akizungumza katika mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19 mjini Dodoma, iliteka mitandao ya kijamii ya nchi hiyo huku maelfu wakichangia kwa kumpongeza na kuiponda Serikali na Bunge lao.
Video hiyo iliyosambazwa na Gavana wa Jiji la Nairobi, Mike Sonko katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook Ijumaa hadi kufikia jana ilikuwa imetazamwa na watu 41,194.
Baadhi ya walioitazama mbali na kumpongeza mbunge huyo, waliwaponda wabunge wa Kenya kuwa hawana uwezo wa kusimama bungeni na kuzungumza mambo yenye masilahi kwa wananchi kama alivyofanya Msigwa.
Baadhi yao walisema wabunge wao wengi ni wabinafsi na wanapigania masilahi yao binafsi.
Katika kile kilichoonekana ‘kuiteka’ nchi hiyo mitandaoni, video hiyo pamoja na habari yenye kichwa cha habari kisemacho “Kwanini mbunge huyu wa Tanzania amewavutia Wakenya”, viliwekwa kwenye tovuti ya Nairobi News (NN) na kunukuu maoni ya wananchi.
Video hiyo inamuonyesha Mchungaji Msigwa akimbana waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuhusu utaratibu wa ulipaji kodi, kusuasua kwa biashara huku akihoji sababu za Serikali ya Awamu ya Tano kuacha mipango mizuri ya kuinua uchumi iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne, ambayo baadhi ilikuwa ikisimamiwa na Dk Mpango kabla ya kuwa waziri.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu maoni yake hayo, Mchungaji Msigwa amesema, “kama ni mtu unayependa udadisi lazima utaupenda mchango wangu. Umekuwa gumzo na nimepokea simu nyingi za pongezi kutoka ndani na nje ya nchi.”
“Dk Mpango kwa kweli anapaswa kujiuzulu maana ni lazima atakuwa ama alimdanganya (Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete au Rais wa sasa (John Magufuli) kuhusu masuala ya uchumi.”
Alichosema bungeni
Akizungumza katika mjadala wa bajeti bungeni, Msigwa alisema, “Rais wetu yeye sio mchumi ni engineer (mhandisi). Tunategemea wewe (Dk Mpango) uliye mchumi umpe maelekezo mazuri ambayo yatasaidia nchi yetu iende, nasikitika sana maana vyanzo vya mapato vya Serikali za mitaa mnavipeleka Serikali Kuu, mnaua hizi halmashauri.”
“Nazungumza kwa masikitiko sana mheshimiwa Mpango, hebu utoe majibu ni uchumi gani unauamini, na nani ulimdanganya kati ya Kikwete na Rais Magufuli? Huu ndio wakati wa Bunge kuibana Serikali maana inalikosea adabu Bunge, inafungua miradi ambayo Bunge haijaianzisha.”
Mbunge huyo aligusia jinsi kodi zinavyoibua msuguano kati ya wafanyabiashara na Serikali, kwamba licha ya Serikali kushauriwa jambo hilo na wabunge miaka mitatu iliyopita, anashangazwa na Dk Mpango kurejea na jambo hilo bungeni katika bajeti ya mwaka 2018/19 huku akiwaponda baadhi ya wabunge waliompongeza waziri huyo na Serikali.
“Huu utaratibu wa uchumi unaokwenda sasa hivi huku mbele tunakwenda kukwama, Dk Mpango utaweka historia maana uchumi sio halisia. Sisi tunaozungumza tunampenda Rais zaidi kuliko wengine wenu huko kwa sababu mnampaka Rais mafuta kwa mgongo wa chupa,” alisema mbunge huyo.
Huku akitolea mfano wa jinsi wanawake wanavyochukua mikopo na kushindwa kuirejesha kutokana na biashara zao kusuasua, Mchungaji Msigwa alisema katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Mpango alikuwa katibu wa Tume ya Mipango, tume ambayo kwa sasa waziri huyo anataka kuifuta.
“Dk Mpango wakati wa Kikwete ulisimamia Kilimo Kwanza, Saggot (Kituo cha Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania), BRN (Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa) na PPP (Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Umma), leo katika Awamu ya Tano umegeuka umekwenda kwenye Stiegler’s Gorge (mradi wa umeme) na ujenzi wa reli ya kisasa na mnachukua mikopo yenye gharama kwa nchi hii,” alisema.
“Sasa tueleze wewe ni mchumi unayeamini nini? Utuambie uchumi wakati wa Kikwete uliokuwa unatengeneza mazingira mazuri ulikuwa na makosa au ulimuingiza chaka, sasa umegeuka. Tunakwenda wapi kama Taifa.”
Alisema wakati wa utawala wa Rais Kikwete, uchumi ulikuwa katika mazingira mazuri na wawekezaji waliletwa kwa wingi nchini lakini sasa kuna uchumi wa kugombana na wawekezaji aliodai wanaonekana wezi na hawalipi kodi.
Ufafanuzi wa ziada
Katika maelezo yake zaidi, mbunge huyo alilieleza Mwananchi kuwa katika mjadala huo alisema wabunge wengi wanashindwa kuwapigania wananchi waliowachagua kwa sababu ya kutotambua wajibu wao.
“Ni makosa ya kutofanyika kwa semina elekezi kwa wabunge. Wengi hawajui kuwa ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) ni jicho la Bunge. Hawajui kuwa kazi yao ni kusimamia Serikali,” alisema.
“Kwa kweli nilimshangaa sana Dk Mpango. Nimeamini wachumi wanakuwa na mambo wanayoyasimamia kulingana na nyakati.”

Comments