Dk. Shein ataka watendaji washuke kwa wananchi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,  ameupongeza uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, kwa kutekeleza vyema majukumu yake na kuutaka kuandaa ziara za kazi kwa ajili ya kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto zinazowakabili.
Hayo aliyasema jana Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa wizara hiyo wakati ilipowasilisha utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2017/2018 na mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2018/2019.
Alisema kwa vile wizara hiyo imeyagusa maisha ya wananchi ni vyema kwa uongozi huo kwenda kuwasikiliza ili kutambua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.
Aliongeza kuwa kumsikiliza mwananchi ni sifa moja wapo ya kiongozi hivyo ni vyema  kwenda kwa wananchi kuwasikiliza hasa ikizingatiwa kuwa wizara hiyo imewagusa wananchi kwa kiasi kikubwa kutokana na huduma zake inazozitoa ikiwemo maji, ardhi, nishati, nyumba na mambo mengineyo.
Aidha, aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa kamati ya uongozi wa wizara hiyo ambayo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na kuwasisitiza wajumbe wa kamati hiyo kuhudhuria vikao husika ambavyo vina umuhimu mkubwa katika kuiongoza Wizara hiyo.
Alieleza umuhimu wa kuzingatia na kufuata sheria na taratibu zinazoongoza wizara hiyo huku akisisitiza haja ya kuwaelemisha wananchi juu ya mambo mbali mbali ya wizara hiyo ambayo wanapaswa wananchi kuyajua zikiwemo sheria za wizara hiyo.
Nae Waziri wa wizara hiyo, Salama Aboud Talib alieleza kuwa  tayari wizara hiyo imekamilisha sera ya ardhi ambayo kukamilika kwakwe kutaiwezesha Zanzibar kuimarisha utawala na maendeleo endelevu ya ardhi na usimamizi wa maliasili zilizomo katika ardhi hiyo kwa ajili ya maendeleo nchini.
Zanzibarleo.

Comments