Mamlaka
ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) imepanga kuondoa
daladala zote zinazosafirisha abiria katika 'ruti' zote za Jiji la
Mwanza, mwakani.
Akizungumza
jijini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe, alisema
mamlaka hiyo imeanzisha mfumo mpya wa usafiri ambapo wamiliki wa
daladala zitoazo huduma sasa jijini hapa wanatakiwa kuungana ili kutoa
huduma hiyo kwa kutumia mabasi makubwa ya usafirishaji kupitia ama
kampuni au ushirika.
Ngewe
alikuwa akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja ya elimu juu ya
utoaji wa huduma ya usafirishaji mijini, kwa kuziondoa daladala na
kutumia usafiri wa mabasi makubwa.
"Serikali
imechukua hatua madhubuti ya kusimamia wamiliki wa daladala kuhakikisha
wanaunganisha mitaji yao na kununua mabasi makubwa ya kutoa huduma
katika jiji hili la Mwanza kupitia makampuni (kampuni) au ushirika,"
alisema Ngewe.
"Tunatarajia
kufikia mwakani 2019 (mwakani) daladala zote ziwe zimeondolewa katika
jiji hili na kuanza kutumia mabasi makubwa yenye kubeba abiria wengi kwa
mara moja."
Ngewe
alisema kuanzishwa kwa mfumo huo mpya jijini Mwanza kutaondoa
changamoto ya msongamano wa magari unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na
daladala.
Alisema jiji hili lina wamiliki wa daladala zaidi ya 2,000 na idadi ya magari 3,400 yanayotoa huduma hiyo.
Kama
mpango huo utatekelezeka, ndani ya miezi sita ijayo Mwanza litakuwa
jiji la pili nchini kuondoa huduma ya usafiri wa daladala baada ya Dar
es Salaam iliyozipunguza kwa kiasi kikubwa katika Barabara za Morogoro
na Kawawa mwaka 2016.
Katika njia hiyo, jiji hilo limeweka mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).
Ngewe
alisema mfumo mpya huo kwa Mwanza utasaidia pia madereva na makondakta
wa daladala za sasa kupata mikataba ya kisheria ya ajira zao na kulipwa
mishahara na mafao ya uzeeni pindi wanapostaafu kazi.
Ngewe
alisema mabasi makubwa yatakayokuwa yakitoa huduma hizo yatatumia mfumo
wa kielektroniki katika utoaji wa tiketi kwa abiria.
Aidha,
mfumo wa kielektroniki utaondoa wizi wa fedha za makusanyo ya nauli za
wenye magari unaofanywa na madereva na makondakta wasio waaminifu,
alisema.
Ngewe
alisema mfumo wa kuungana mitaji kwa wamiliki kupitia kampuni au
ushirika ili kuendesha biashara ni mzuri kwani utawasaidia kupata mikopo
ya kifedha kwa urahisi, kukuza mitaji na uchumi kuliko umiliki wa mtu
mmoja mmoja.
Mafunzo
hayo yalihusisha viongozi wa usalama barabarani, wamiliki wa daladala
za abiria mijini, viongozi wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua) na wadau
mbalimbali wa usafirishaji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Credit: Nipashena Mpekuzi.
Comments