Balozi Seif: Kuna mafanikio utekelezaji ilani.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema uagizaji wa bidhaa ikiwemo chakula na matunda kutoka nje ya Zanzibar umepungua kutokana na wakulima nchini kuhamasika katika kilimo.
Balozi Seif alieleza hayo wakati alipofanya mahojiano maalum na timu ya wanahabari wa habari kutoka Redio Uhuru na magazeti ya Chama cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo.
Timu hiyo ya waandishi iliomba kukutana na Balozi Seid Ali Iddi kutaka kujua utekelezaji wa ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar, ambapo mahojiano hayo yalifanyika katika ofisi ya uratibu wa SMZ jijini Dar es Salaam.
Balozi Seif alisema sekta ya kilimo ni miongozi mwa maeneo yaliyopewa msukumo wa kwanza na CCM wakati kikiomba ridhaa ya kutaka kuongoza dola ya Tanzania kwenye kampeni za uchaguzi mkuu kilipotangaza sera na ilani yake.
Alisema kutokana na serikali za CCM kusamehe ushuru wa forodha kwenye vifaa vya kilimo vinavyoingizwa nchini sambamba na kuendeleza mafunzo ya kisasa kwa wadau wa kilimo, wakulima wengi nchini wanaojishughulisha na kilimo cha matunda wameongeza uzalishaji.
Balozi Seif alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, wakulima wamekuwa wakilalamikia ufinyu za soko la bidhaa wanazozalisha jambo ambalo imefikia wakati baadhi ya bidhaa hizo zikisafirishwa kupelekwa upande wa Tanzania bara.
Akigusia sekta nyengine za kiuchumi akitolea mfano zile za utalii, viwanda, elimu, afya na miundombinu ya mawasiliano ya barabara na anga, Balozi Seif alisema serikali chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein imeweza kupiga hatua kubwa katika uimarishaji wa miundombinu kwenye maeneo hayo.
Zanzibzr24.

Comments