Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison
Mwakyembe amewataka walimu wa michezo nchini kutumia michezo ya UMISSETA
na UMITASHUMTA kuibua vipaji kupitia hazina ya vijana wadogo waliopo
katika shule za msingi na sekondari wenye uwezo mkubwa katika michezo
mbalimbali.
Rai hiyo ameitoa jana Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao na wadau
wa sekta ya michezo kujadili namna ambavyo michezo ya UMISSETA na
UMITASHUMTA itakavyoendesha mwaka huu ambapo michezo hiyo inatarajiwa
kufanyika kuanzia mwezi Juni mwaka huu Jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewataka wadau wa michezo nchini kujitokeza
kwa wingi kuchangia ili kufanikisha michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA
na kuifanya michezo hiyo kuwa agenda kubwa hapa nchini katika kuendeleza
michezo na kuinua vipaji vya michezo mbalimbali.

Aidha Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania
(TUCTA) Dkt. Yahya Msigwa amesema kuwa Michezo ni kila kitu katika jamii
kwani michezo ni ajira, michezo ni siasa, michezo ni kinga dhidi ya
ukimwi na kinga dhidi ya ujambazi kwa vijana, michezo ni biashara,
michezo ni utamaduni na pia michezo haina mipaka kati ya nchi na nchi.
“Kama tunataka kweli mabadiliko chanya katika michezo ni
lazima tuanze na watoto waliopo katika shule za msingi na sekondari ili
tuweze kuwajengea uwezo na kuimarisha michezo kwani huko ndiko chimbuko
la michezo linapoanzia” amesema Dkt. Msigwa.
Naye mwakilishi kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Bw. Maganga
Japhet amesema kuwa wadau wa michezo nchini wanapaswa kusaidiana kwa
pamoja na serikali katika kuboresha mkakati huu wa kuibua, kukuza na
kuendeleza vipaji kupitia michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwani kwa
kufanya hivyo kutalifanya taifa kuwa na wachezaji wazuri walioandaliwa
kuanzia ngazi ya chini.


Zanzibar24.
Comments