Licha ya kuwa Zanzibar ni miongoni mwa sehemu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzani lakini inayo mamlaka ya kujiamulia mambo yake hususani yanayohusu uongozi.
Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar wananchi wa visiwa hivi hulazimika kuchagua viongozi wawapendao kila baada ya miaka mitano kwa kupitia uchaguzi mkuu ambao huandaliwa na kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa nafasi ya ubunge.
Imani na matumaini ya wengi na ndivyo ilivyo ni kwamba hakuna njia mbadala ya kupatikana viongozi wa nchi kinyume na uchaguzi ambao ndio unaowapa wanachi fursa ya kuamua nani wanamtaka na nani hawamtaki.
Lakini swali kubwa la kujiuliza ni je dhamira ya walio wengi juu ya maendeleo kutoka kwa viongozi wao hutimia?
Je waliopewa dhamana ya uongozi wakiwamo wabunge na wawakilishi kupitia masanduku ya kura wanatekeleza wajibu wao kwa wananchi.
Nilifunga safari hadi kijiji cha Uchukuni shehia ya Machui Wilaya ya Kati Unguja ili kujionea ni kwa namna gani waliopewa dhamana wanatekeleza wajibu wao kwa wananchi walioamua kuwapa ridhaa zao ili wawalipe maendeleo.
Hali inasikitisha kwenye eneo hili, ni kama vile wananchi wa eneo hili hawana viongozi waliowachagua, kuna tatizo kubwa la ukosefu wa huduma muhimu za kijamii.
Kwenye kijiji cha Uchukuni chenye wakazi takriban 150, huduma ya maji safi na salama imeendelea kuwa ndoto ya muda mrefu.
Wananchi wanatumia maji yanayotoka kwenye visima visivyo salama, yeyote atakayefika ndani ya kijiji hicho anaweza kushangaa hali atakayokutana nayo.
Wakazi wa kijiji hicho wanasema wamekua wakitumia maji yasiyo salama kutoka katika kisima cha kijijini hapo kwa kuwa hawana mengine tangu wameanza kuishi katika kijiji hicho miaka ya 1960.
Mwaka Msabah mama wa makamo wa kijiji hicho anasema anachoamini hadi sasa ni majaliwa tu ya Mwenyezi Mungu yanayowafanya wasipate magonjwa kwa kutumia maji hayo.
Anadai eneo hilo ni kama maeneo mengine yenye wananchi wanaostahiki kupewa haki zote za msingi ikiwemo huduma ya maji, wenye wajibu wa kufanya wafanye wasisubiri kukumbushwa.
Kijiji cha Uchukuni pia kina tatizo kubwa la shule, watoto wa kijiji hicho hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Wazazi wanasema watoto wao hulazimika kutembea zaidi ya saa mbili kwa kwenda na kurudi shule jambo ambalo huwaweka watoto hao katika mazingira hatarishi ikiwamo kubakwa na mengineyo.
Hussan Mohamed ni mmoja wa mama wenye watoto anayeishi kwenye kijiji hicho, anasema amekua akipata shida kumuandaa mtoto wake mapema ili awahi shule.
Anasema kwa muda wote mtoto wake tangu anatoka hadi anarudi amekua akiishi kwa hofu akitafakari njia anazopita wakati wa kwenda na kurudi shule.
Anaamini katika elimu kwa wote na hivyo anasisitiza juu ya kujengewa shule kwenye eneo lao ili waepukane na changamoto hiyo kwa watoto wao.
Huduma za afya
Mbali na elimu wananchi hao pia wanakabiliwa na tatizo la huduma za afya.
Mkazi mwingine Haji Machano Silima anasema ukosefu wa huduma bora za afya ni changamoto ya muda mrefu katika kijiji chao.
Anasema bado kuna tatizo kubwa kwa viongozi wao ambao alidai iwapo watatimiza wajibu wao huenda kijiji chao kikawa miongoni mwa vijiji vitakavotajwa kwa sifa njema kiafya.
Anasema mara nyingi wamekuwa wakiomba dua uda wa kina mama wajawazito kujifungua uwe mchana ila inapotokea kuumwa uchungu usiku ni shida kwa kuwa kituo cha afya wanachokitegemea kipo mbali.
Silima anasema barabara kuu ya Machui hadi Uchukuni ni kama mwendo wa saa moja na robo 15 kwa usafiri wa gari iwapo njia yake ingekua nzuri.
Akiongezea uzito kuhusu tatizo hilo Jena Machano anasema hatasahau maishani mwake mkasa uliomfika wa kujifungua njiani.
Anasema alilazimika kujifungua njiani kutokana na ubovu wa njia hiyo wakati alipokua akijaribu kwenda kituo cha afya lakini hakufanikiwa na hivyo alilazimika kujifungua njiani.
Uchumi wa kilimo
Kwa upande wake Machano Ali anaamini kuwa miundombinu ya barabara ikipatikana kwenye eneo lao itasaidia pia kukuza uchumi wa eneo hilo ikiwemo kusafirisha bidhaa zao za kilimo kwa wakati muafaka kwenda sokoni.
“Eneo letu hili tunajihusisha zaidi na kilimo lakini kilimo huishia hapa hapa, tunashindwa kuuza mazao yetu mjini kwa wakati muafaka kutokana na njia yetu kutokua rafiki,’’ anaongezea Ali.
Sheha wa shehia hiyo, Mussa Miraji Faizi anatambua uwapo wa changamoto hizo na mara kadhaa wamekuwa wakifanya jitihada mbali mbali ili kutatuliwa.
Akitaja miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kufika ofisi za mkuu wa wilaya na tayari alishafanya mkutano na wananchi wa shehia hiyo juu ya kero zao.
Anasema kadhia hizo za wananchi wa eneo hilo zilimgusa mkuu wa wilaya na kuahidi mara tu miradi ya maendeleo itakapofikia wilayani kwake atahakikisha kijiji hicho kinatazamwa kwa jicho la pekee.
Akizungumzia changamoto za kijiji hicho mkuu wa mkoa Kusini Unguja, Hassan Khatib Hassan amesema anazifahamu changamoto za mkoa wake zikiwamo za kimaendeleo katika kijiji cha Uchukuni hasa tatizo la maji na kituo cha afya.
Anasema Serikali kupitia mkoa imeshafika eneo hilo na juhudi za utatuzi wa baadhi ya changamoto zipo katika hatua nzuri. “Tumedhamiria kijiji hicho nacho kukifanya kuwa ni kijiji ambacho kina huduma za kijamii kama vilivyo baadhi ya vijiji, tumepanga miradi ambayo italengwa kufanyika ndani ya mkoa wetu huu ianzie katika kijiji hicho,” amesema.
Aliwataka wananchi wa kijiji hicho waendelee kuwa na subra huku Serikali yao ikifanya juhudi kuhakikisha inatekeleza kikamilifu sera ya maisha bora kwa wananchi wake.
Kwa upande wake mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) Dk Alley Soud anasema mara nyingi kiongozi anaposhindwa kuteleleza wajibu wake kwa wananchi waliomchagua huibua matabaka ya pande mbili na miongoni mwao huzaa chuki ambazo huibua pia mgogoro wa ndani ya nafsi zao.
Anasema iwapo kiongozi atashindwa kutekeleza wajibu wake hali hiyo pia huwa sababu ya wananchi au wanachama wa chama chake kumchukia yeye na chama chake wakati mwingine hata kumyima kura na kiujumla hali hiyo inachangia kuzorota maendeleo ya nchi.
“Pita katika baadhi ya majimbo leo utakuta vijana wengi hawana kazi ambazo naamini kama wangeratibiwa vizuri na kukusanywa pahali pamoja wangeweza kuunda vikundi vyao vya ujasiriamali na kujipatia kipato chao wenyewe ili kuipunguzia Serikali mzigo,” anaongeza mhadhiri huyo.
Pamoja na hayo Dk Alley pia anaamini kwamba muda bado upo kwa wanasiasa hao kujitafakari na kuwalipa maendeleo wananchi waliowachagua.
Kwa kwa kuwa Zanzibar ni sehemu yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa wa vyama viwili ambavyo ni CCM na CUF huku kila chama kikiwa na ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015 na kujinasibu hadharani ni vipi ilani hizo zitatekelezwa kivitendo.
Miongoni mwa yaliyosisistizwa kwenye ilani za vyama hivo wakati wa kampeni ni pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ya ubaguzi ikiwemo huduma ya maji safi na salama kwa kila mwananchi mijini na vijijini.
Lakini kilio hicho hadi sasa bado kinaedelea kutiririka kwenye nyuso za kinanama wanyonge waliokosa wa kuwatetea hadi leo hii wakiwamo hawa wa Kijiji cha Uchukuni. Enzi za uhai wake Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume alipata kusema: “Utumishi wa umma ni kazi ya kujitolea si sehemu ya kujilimbikia fedha’’
Kauli hii ni kama inaendelea kuishi hadi leo hii ikiwakumbusha wanasiasa kutekeleza wajibu wao kwa wananchi na si kujilimbikia mamilioni ya fedha na wengine hata kuyakimbia maeneo waliyopewa ridhaa ya kuyaongoza.
Mwananchi.
Comments