Spika
wa Bunge, Job Ndugai ameishukia Serikali kuhusu madai ya kupanda kwa
bei ya mafuta ya kula akimtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage kufikia leo Jumanne Mei 8, 2018 saa 11 jioni
kuwasilisha bungeni taarifa ya kinachoendelea kuhusu jambo hilo ili
kuondoa sintofahamu kwa wananchi.
Ndugai
ametoa kauli hiyo leo asubuhi bungeni mjini Dodoma wakati akijibu
mwongozo wa mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe aliyehoji kuhusu
bei ya mafuta, akidai imepanda na kujibiwa na Mwijage kuwa jambo hilo
linashughulikiwa kwa maelezo kuwa kwa sasa umeibuka mvutano.
Tishio
la kuadimika kwa mafuta ya kula linatokana na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kuzizuia meli mbili zenye tani 62,000 za mafuta ya kula
katika Bandari ya Dar es Salaam tangu mwezi uliopita kushusha mzigo
mpaka wamiliki wake watakapolipa kodi husika.
Utata
wa kulipa kodi inayodaiwa na TRA, unatokana na madai ya mamlaka hiyo
inayosema mafuta yaliyoingizwa ni safi ilhali wamiliki wakieleza ni
ghafi.
Leo
katika majibu yake, Mwijage baada ya kutoa maelezo marefu amesema
alitoa ushauri kwa TRA kwamba wenye mafuta, “nusu ya mzigo ushushwe,
tatizo linalokuja tunahukumiwa na historia, nashauri hii kazi unipe
mimi, nitakuja saa 11 kukueleza kipi kimetokea.”
Baada
ya kauli hiyo ya Mwijage, Spika Ndugai alisimama na kusema: “Nalikubali
hili la saa 11 na bahati nzuri nitakuwa hapa. Tunapokuwa bungeni lazima
tuseme ukweli yaani iko hivyo.Tukiligeuza Bunge hili kuwa mahali pa
kubangazia hivi, mimi niombe saa 11 tupate majibu ya uhakika.”
“Mnatufikisha
mahali pagumu sana, kwa mambo madogo mno, hivi tuliosoma kemia hivi
kupima mafuta kujua ni ghafi au masafi inachukua muda? Kitu cha dakika
kumi na tano watu wanazunguka zunguka. Hamuwamini TBS (Shirika la
Viwango Tanzania) au pelekeni Nairobi, Afrika Kusini, Kenya mnapima na
kupiga kodi.”
Huku
akishangiliwa Ndugai amesema, “…tunaumiza wananchi na hata yakikaa huko
yakiingia anayeumia ni mwananchi, sisi tunalumbana tu.”
Awali,
baada ya majibu ya Mwijage, Ndugai alimtaka mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Suleiman Saddiq kulielezea
suala hilo na kusema walipokutaka katika semina Jumamosi iliyopita,
lilijitokeza ukiwamo mkanganyiko kati ya TBS, TRA na Mkemia Mkuu wa
Serikali.
Baada
ya Ndugai kueleza msimamo wake kuhusu jambo hilo, Mwijage alinyanyuka
alipokuwa ameketi kwenda kuteta na waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Jenista Mhagama kisha kwa pamoja kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Mpekuzi.
Comments