Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameagiza uandaliwe
mkataba wa makubaliano ya awali (MoU) ya utekelezaji wa mradi wa
kuendeleza utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.
Mkataba
huo wa makubaliano utahusisha wawekezaji kutoka Jiji la London nchini
Uingereza na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania TAWA na utakapokamilika utasainiwa na pande zote
mbili.
Dk.
Kigwangalla ametoa agizo hilo juzi ofisini kwake Jijini Dodoma kufuatia
maombi yaliyowasilishwa kwake na wawekezaji hao, Eva Sanchez na
Nicholas Negre.
Akiwasilisha
maombi hayo, Sanchez amesema mradi huo utakuwa wa ubia na Serikali ya
Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA ambao
ndio wasimamizi wakuu wa Pori la Akiba Selous utakapoanzishwa mradi
huo.
Amesema
pamoja na mambo mengine mradi huo wa utalii wa picha pia utasaidia
kupiga vita ujangili na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka pori hilo.
Dk.
Kigwangalla amewataka wawekezaji hao kuwasilisha andiko la mradi huo,
kufanya utafiti wa kina na tathmini ya athari za kimazingira
zitakazoweza kujitokeza kutokana na uanzishwaji wa mradi huo.
Amesema
kwa sasa Serikali inafanya marekebisho ya Sheria mbalimbali
zitakazoiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA
kutekelezaji majukumu yake ipasavyo ikiwemo uwekezaji wa aina hiyo
kwenye sekta ya Utalii wa Picha na Uwindaji wa Kitalii.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara amesema mamlaka hiyo itatoa
ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji hao ili kutimiza azma ya Serikali
ya kushirikisha wadau, watu binafsi na wawekezaji katika kukuza sekta ya
utalii nchini.
Pori
la akiba Selous ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini ikiwa na ukubwa
wa kilomita za mraba takriban 50,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro,
Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mwaka 1982, Shirika la Umoja wa Mataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni (Uneso) lilitangaza eneo hilo kuwa moja ya
eneo la Urithi wa Dunia na kuanza kuhifadhiwa.
Mpekuzi.
Comments