
Katika maadhimisho hayo, Dk. Shein anatarajiwa kupokea maandamano ya
wafanyakazi wa sekta za umma na sekta binafsi ambapo pia, salamu mbali
mbali zitatolewa zikiwemo kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Jumuiya
ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA), salamu za Waziri, Mkuu wa Mkoa, risala ya
wafanyakazi na hatimae, Rais atatoa zawadi na kuwahutubia wafanyakazi.
Kila ifikapo Mei Mosi ya Kila mwaka, Zanzibar huungana na nchi
nyengine duniani katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo
hapo mwaka jana maadhimisho hayo yalifanyika katika kiwanja cha Mpira
Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo inasema ‘Njia Pekee
ya Kukuza Uzalishaji na Kuimarisha Huduma ni Kujadiliana na Kujali
Ushirikishwaji”.
Katika hotuba zake mbali mbali anazotoa Rais Dk. Shein amekuwa
akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na
utaratibu wake wa kuzilinda haki za wafanyakazi na kuimarisha maslahi ya
wafanyakazi hatua kwa hatua.
Katika hotuba yake ya kuzindua Baraza la Nane la Wawakilishi tarehe
11 Novemba mwaka 2010 Rais Dk. Shein alieleza bayana mtazamo wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kuhusu wafanyakazi ambapo
alisema “Rasilimali moja kubwa ya nchi ni wafanyakazi ambapo ndio msingi
wa kujenga uchumi na maendeleo yote ya nchi”.
Aidha, katika kutilia mkazo suala la umuhimu wa kushirikiana na vyama
vya wafanyakazi alisema kuwa “ Maslahi bora ya wafanyakazi popote ni
ajenda yetu na tutahakikisha mashirikiano na chombo chao ‘Shirikisho la
vyama huru vya wafanyakazi’ na kukuza mahusiano mema”.
Kama inavyofahamika kuwa wafanyakazi ni muhimu katika maendeleo ya
Taifa lolote lile kwani ni rasilimali inayotegemewa katika kuzalisha
mali na kunyanyua uchumi wa nchi.
Kwa kutambua hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua
hatua mbali mbali kujenga mazingira mazuri kwa wafanyakazi ili waweze
kuzalisha zaidi na kuongeza pato la Taifa.
Siku hii ya Mei Mosi inatokana na historia ya maandamano yaliyotokea
Chicago nchini Marekani mnamo mwaka 1886 ambapo zaidi ya wafanyakazi
300,000 waliandamana wakidai haki zao za msingi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Zanzibar24
Comments