Wanawake 10 wapigwa na waume zao.

KESI 10 za wanawake kupigwa na waume zao zimeripotiwa katika Mkoa wa Kusini Unguja kwa mwaka jana pekee.

Wakizungumza, baadhi ya wanawake wa mkoa huo, walisema licha ya juhudi zinazochukuliwa na wanaharakati wa kutetea haki za wanawake ili kukomesha vitendo hivyo, bado baadhi ya watu wanaendelea kuwapiga wanawake.

Wakiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mpango kazi kuhusu vitendo vya udhalilishaji, walisema sababu ya wanawake kupigwa zinatokana na ulevi wa waume zao na wivu wa mapenzi.

Akizungumza katika kikao hicho kilichoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), mwanaharakati Zimba Khatib, alisema baadhi ya wanaume wanaowapiga wake zao ni walevi kupindukia na wengine wamekithiri kwa wivu.

Alisema wengi wa wanawake wanaopatwa na kadhia hiyo hawaripoti kesi hizo kwa kuhofia kuachwa.

Alisema ili kupunguza tatizo hilo jamii bado inahitaji elimu ya kufahamu haki zao na kuchukua hatua pale vitendo hivyo vinavyowapata.

“Hali duni za maisha walizonazo wanawake pia zinachangia kudhalilishwa kijinsia ikiwemo kupigwa na waume zao kutokana na kuwategemea kwa kiasi kikubwa wanaume,” alisema.

Bahati Issa, Katibu mtandao wa ardhi wilaya ya kati, Mkoa wa Kusini Unguja, alisema licha ya Mkoa huo kushamiri kwa vipigo lakini pia bado watoto wanafanyiwa udhalilishaji.

Nae Meneja utetezi kutoka Tamwa Zanzibar, Hawra Shamte, alisema Tamwa inaridhishwa na utendaji kazi wa wanaharakati hao wa kuibua changamoto nyingi katika jamii.

chanzo: zanzibarleo.

Comments