Serikali
ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kiuchumi wa Kuwait (Kuwait for
Arab Economic Development Fund), na Serikali ya Tanzania zimetiliana
saini rasimu ya mkataba wa kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti
nafuu wa dola milioni 15.3, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 34, kwa
ajili ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Luiche, mkoani
Kigoma, lenye ukubwa wa hekta 3,000.
Rasimu
hiyo ya Mkataba imesainiwa na Kiongozi wa ujumbe wa wataalamu na
Mshauri wa Masuala ya Kilimo wa Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa
Kuwait, Dkt. Abdulrida Bahman na kwa upande wa Tanzania ikisainiwa na
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu,
mjini Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) amesema hatua
hiyo imfikiwa baada ya timu ya wataalamu kutoka Kuwait kutembelea eneo
la mradi mkoani Kigoma na kuridhishwa na umuhimu wake kiuchumi kwa
wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
“Mradi
huo una umuhimu mkubwa kwa watanzania kwa kuwa wataweza kuwa na kilimo
cha umwagiliaji cha Mpunga na Mbogamboga kwa mwaka mzima badala ya
kilimo cha msimu cha kutegemea mvua, na katika siku zijazo Kigoma itakua
miongoni mwa mikoa inayozalisha mchele kwa wingi”, alisema Dkt. Mpango.
Dkt.
Mpango amesema kuwa Serikali ya Tanzania na Kuwait zitatia saini
mkataba rasmi wa mkopo huo wenye masharti nafuu ifikapo mwishoni mwa
mwezi Juni mwaka huu ili mradi huo uanze kutekelezwa ili kuongeza kipato
cha wananchi na kuwa na uhakika wa chakula.
Amesema
Nchi ya Kuwait imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kutekeleza miradi
mbalimbali ikiwemo ya ukarabati wa Hospitali ya Mnazi mmoja, Zanzibar
kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 13.6 sawa na shilingi bilioni 31.
"Kwa
upande wa Tanzania Bara wametoa mkopo nafuu wa shiingi bilioni 115 kwa
ajili ya kuboresha barabara ya Chaya hadi Nyahua (km 85) kwa kiwango cha
lami ambayo ni muhimu kwa kuwa inaunganisha mikoa ya Magharibi mwa
Tanzania" aliongeza Dkt. Mpango
Miradi
mingine ambayo nchi hiyo imeonesha nia ya kuisaidia nchi, ni pamoja na
ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, uboreshaji
wa barabara ya kutoka Morogoro hadi Dodoma na ujenzi wa barabara za
mzunguko za kuingia na kutoka mjini Dodoma ambazo zitasaidia kuondoa
msongamano wa magari yanayopita katikati ya mji huo kutokana na
kuongezeka kwa idadi ya watu na vyombo vya moto baada ya Makao Makuu ya
Serikali kuhamia Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Mpango ameishukuru nchi ya Kuwait kupitia
Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait, kwa nia yake njema na thabiti
katika kusaidia nchi ya Tanzania kutekeleza kwa mafanikio miradi ya
Maendeleo ya kiuchumi katika nia yake ya kupata maendeleo Stahiki.
Kwa
upande wake Kiongozi wa ujumbe wa wataalamu na Mshauri wa Masuala ya
Kilimo wa Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait, Dkt. Abdulrida
Bahman, ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Fedha na
Mipango kwa ukarimu pamoja na Idara ya Taifa ya Umwagiliaji kwa
ushirikiano mzuri katika hatua za kufanikisha utekelezaji wa mradi wa
umwagiliaji wa Bonde la Luiche, Mkoani Kigoma.
“Tumetembelea
eneo la mradi kwa takribani wiki mbili tumejionea uzuri wa nchi hii na
fursa zilizopo, hii ni nchi tajiri na inaweza kuwa tajiri kuliko Kuwait
kwa kuwa kila kitu kinachoweza kufanya nchi hii iwe tajiri
kipo”.Alieleza Dkt. Bahman.
Amesema
mradi huo wa umwagiliaji hautakuwa wa mwisho kupewa fedha na mfuko huo
bali utaendelea kusaidia kutekeleza miradi mingine mingi kama ilivyokuwa
ikifanya, kutokana na ushirikiano mzuri, wa kihistoria, na wa muda
mrefu kati ya nchi hizo mbili.
chanzo:Mpekuzi.
Comments