SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema
kuwa inafuatilia kujua ukweli kama ZFA ilitumiwa barua ambayo, imetoa
muongozo wa umri kwa timu shiriki katika michuano ya CECAFA
inayoendelea nchini Burundi.
Hatua hiyo ya Serikali imekuja baada
ya timu ya Taifa ya vIJANA Zanzibar U-17 (Karume Boys) kuondolewa
kwenye michuao ya Chalenji ya Vijana kwa madai kuwa imepeleka vijana
waliozidi umri.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Omar
Hassan (King), alisema kuwa pamoja na wao kufuatilia lakini inaitaka ZFA
nayo kufuatilia njia za mawasiliano, ili kujua kwamba barua hiyo
ilitumwa au la.
Alisema kuwa ikiwa ZFA itabainika
walitumiwa barua hiyo na kusindwa kuitafsiri au kuisoma, ni muda wa
chama hicho kuiangalia katiba yao na kujitathmini ili kuweza kuachia
ngazi.
Alisema kuwa Serikali inafuatilia
kuhakikisha kwamba ni kweli barua hiyo ilitumwa na wakiibaini kama kuna
uzembe umefanyika Serikali itatoa maamuzi.
Hata hivyo alisema kwamba kwa wakati
huu, wametoa muda kwa chama hicho kufuatilia CECAFA na baadae kuja na
majibu ambayo watayapeleka Serikalini ili waweze kuchukua hatua.
“Licha ya kuwa tunaiachia ZFA lakini
tunafuatilia ila mpaka leo (jana) tulipowauliza ZFA wanasema
hawajatumiwa, sisi tunawapa muda waangalie njia za mawasiliano
zilizotumika kutoka kwa Katibu mkuu wa CECAFA”, alisema.
Aidha alisema kuwa katika hilo Serikali itatoa majibu yake ndani ya mwezi mmoja ingawa alisema kuwa hawana
uwezo wa kuwawajibisha viongozi hao kutokana kuwa ni chama huru na wao
wana utaratibu wao ila kwa katibu ambae yupo chini yao wakibaini
watachukua hatua ambazo zitawaridhisha wote.
“Ikiwa tutabaini kwamba wametumiwa
barua na wameshindwa kuzifuata kazi yetu tutawapa ushauri na wao wenyewe
watajithmini ili waweze kuachia ngazi, lakini sidhani kwamba ndio sisi
tumekuwa vilaza wa aina gani ili tuweze kushindwa kutafsiri vigezo na
kanuni zlizotumwa katika barua hiyo”alisema.
Juzi Zanzibar ilitangazwa kutolewa
kwenye mashindano hayo ambayo yanashirikisha vijana waliochini ya miaka
17 yanayofanyika nchini Rwanda kwa madai kuwa wameingiza wachezaji
kinyume na muongozo uliotolewa na waandaaji wa mashindano hayp.
Katibu mkuu wa Wizara hiyo Omar Hassan
(King) ametoa ufafanuzi huo mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu kadhia
hiyo, ambayo imegusu nyoyo za Wanzabari wengi waliohuzunishwa na jambo
hilo.
Alisema endapo itathibitika kuwa Chama
cha Soka Zanzibar (ZFA) ndio wenye makosa mpaka hadi Karume Boys
kuondolewa katika Mashindano basi vyema wakawajibika kwa kujiuzulu.
Zanzibar iliondolewa katika Mashindano
hayo na kupigwa faini kwa kosa la kuorodhesha wachezaji waliozaliwa
kabla ya 01/01/2002 ambapo kanuni ya Mashindano hayo iliwataka wachezaji
waliozaliwa tarehe hiyo, lakini Zanzibar ilipeleka wachezaji 12
waliozaliwa 2001, jambo ambalo ZFA wamesema hawana taarifa kama
wachezaji waliotakiwa ni wale waliozaliwa 2002.
Zanzibarleo.
Comments