Serikali haina mpango kurudisha ardhi kwa wananchi.

Serikali imesema haina mpango wa kurejesha kwa wananchi eneo la ardhi katika Gereza la Matongo kama ilivyoombwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema leo Aprili 19 bungeni na kueleza kuwa  gereza hilo lililopo mkoani Simiyu katika Wilaya ya Bariadi lenye ukubwa wa eka 2,472.62 bado lina umuhimu wake hasa katika shughuli za kilimo.
Masauni amesema gereza hilo lilianzishwa mwaka 1975 kwa kuchukua eneo lililokuwa la mbunge wa zamani wa Bariadi, Edward Ng'wani (marehemu) ambaye alifidiwa eneo jingine la Serikali.
Awali, Chenge aliiomba Serikali kama itakuwa tayari kurejesha eneo la gereza hilo kwa wananchi wa vijiji vinavyolizunguka.
Naibu Waziri Masauni amesema wananchi wa vijiji vya Mwanchumu na Salaliya kwa asili yao si wenyeji, bali ni wahamiaji kutoka maeneo mengine.
Amesema Serikali ilitwaa eneo hilo ili kuliwezesha Jeshi la Magereza kuendeleza shughuli za urekebishaji tabia wafungwa na mahabusu.

Comments