Katika hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na waziri wa Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Castico kwenye
maadhimisho ya siku ya mtoto yatima duniani huko Fumba, Samia amesema
kuwapuuza yatima ni kubeba dhima kwa Mwenyezi Mungu.
Alifahamisha ni lazima ndugu na wanafamilia wa wazazi wanaotangulia
mbele ya haki, wakubali kuwa walezi wa watoto wanaoachiwa kwa kila hali
na kuwapatia mahitaji ya msingi ikiwemo elimu na kuwafundisha maadili
mazuri.
Makamu wa Rais, alieleza kuwa, haijuzu kwa mtu mzima kupuuza umuhimu
wa kuwalea na kuwatunza watoto yatima, ikizingatiwa kwamba kila mmoja
atakutana na kifo wakati wowote, hivyo naye pia kuacha watoto nyuma
yake.
“Unapomnyanyasa yatima wa Mungu, ukamnyima matunzo, na mara nyengine
ukamdhulumu mirathi na haki zake wakati nawe pia una watoto, na ni mgeni
katika dunia hii, je, ukifariki utaridhika watoto wako wanyanyaswe?”,
alihoji Makamu wa Rais.
Alisisitiza kuwa, jukumu la kuwalea na kuwatunza watoto waliopoteza
wazazi wao ni la kila mtu na wanapaswa kuwapa upendo, matunzo pamoja na
elimu ambayo ndio mkombozi wa maisha yao kwa sasa na hapo baadae.
Alitumia nafasi hiyo kuipongeza jumuiya ya Muzdalifah inayolea watoto
yatima ambayo ndiyo iliyoandaa maadhimisho hayo, kwa juhudi kubwa
inazochukua kuwalea na kuwasomesha watoto.
Alisema hakuna kitu chenye thamani cha kumrithisha mtoto kama elimu,
ambayo hata maandiko ya vitabu vitakatifu yanahimiza watoto kupatiwa
rasilimali hiyo kwa jitihada zote.
Aidha aliwahimiza watoto kutekeleza wajibu wao wa kuishika elimu,
akisema ndio ufunguo wa mafanikio katika maisha yao, sambamba na
kuwapongeza baadhi yao waliofanya vizuri katika mitihani ya taifa ya
kidato cha nne mwaka 2017.
chanzo: zanzibarleo.
Comments