Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeeleza kutofurahishwa na kupungua kwa bajeti ya mishahara kwa watumishi wa Mahakama wakiwamo majaji ingawa idadi yao imeongezeka.
Maoni hayo yamekuja muda mfupi baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuwasilisha mpango na makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Kamati ya Bunge ya Bajeti katika maoni yake kuhusu bajeti hiyo ilisema bajeti ya mishahara ya watumishi hao kwa mwaka huu wa fedha,imepungua kwa asilimia 3.3.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Rais wa chama hicho, Fatma Karume alisema bajeti ya mwaka jana ilikuwa Sh 56.4 bilioni na kwamba mwaka huu imeshuka hadi Sh 54 bilioni.
Akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2018/19, Waziri Kabudi alisema majaji wapya 12 wameongezwa.
“Matumizi mengineyo yamebaki hivyo hivyo lakini kitu kilichopanda ni fedha za miradi ya maendeleo,” alisema.
Alisema fedha za maendeleo zimepanda kutoka Sh18 bilioni hadi Sh36 bilioni katika bajeti ya mwaka ujao.
Hata hivyo, alisema fedha zinazotokana na mapato ya ndani za kugharimia miradi ya maendeleo zimepungua kutoka Sh17 bilioni kwa 2016/17 hadi kufikia Sh15 bilioni kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Fatma alisema fedha za miradi ya maendeleo kutoka nje ya nchi mwaka 2017/18 zilikuwa Sh1 bilioni na zimepanda hadi kufikia Sh21 bilioni 2018/19.
“Kwenye matumizi ya maendeleo, fedha za ndani zimeshuka sana na wanategemea fedha za wahisani,” alisema.
Alisema bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 Sh125 bilioni ziliidhinishwa lakini zilizotolewa ni Sh77 bilioni.
Alisema hali si nzuri na maisha yanapanda huku kesi zikiongezeka.
“Watu wengi wananiuliza kwa nini kesi zinachelewa, zitaendelea kuchelewa kwa sababu fedha zinazoombwa na Mahakama hazipatikani zote,” alisema.
Kuhusu mawakili sita waliosimamishwa kazi ya uwakili, Fatma aliwataka Watanzania kutokosa Imani na mawakili kwa sababu hiyo ni idadi ndogo ya mawakili.
“Nidhamu ya wakili ni kitu muhimu sana. Lakini hawa waliobainika ni chini asilimia 0.05 ukilinganisha na idadi ya mawakili waliopo nchini, kwa hiyo si tatizo kubwa. Bahati mbaya mema hayasemwi, ninawaomba tu wasipoteze imani na wanasheria,” alisema.
Alisema uchambuzi huo ni kama utangulizi na kwamba baadaye watachambua bajeti za Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mwananchi
Comments