Mwenyekiti
wa Bunge, Mussa Zungu, amemzuia Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo
Peneza, kuchangia bungeni baada ya kuendelea kulitaja jina la Rais
wakati wa kuchangia kwake licha ya kukatazwa kufanya hivyo.
Upendo
alikuwa akimhusisha Rais na kuzuiwa kwa maandamano nchini na matangazo
ya moja kwa shughuli za chombo hicho cha kutungwa sheria, yaani ‘Bunge
Live’.
Kutokana
na mbunge huyo kumtaja Rais katika mchango wake, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama, aliomba kutoa taarifa ya kukiukwa kwa kanuni za 68(1)
na 64(1) za Bunge akieleza kuwa Rais anawakilishwa na mawaziri ndani ya
Bunge kwa mujibu wa Katiba.
“Na
kanuni hii ya 64 inatukumbusha kwamba, haturuhusiwi kuzungumza mwenendo
wa Rais na hasa anapokuwa katika madaraka ndani ya ofisi yake,”
alisema.
Mhagama
pia alisema hawatakiwi kuzungumza jina la Rais kutaka kushawishi namna
ya kutoa uamuzi na kwamba kama Peneza anaona kuna shida azungumze na
wawakilishi wake.
Akitoa
majibu ya mwongozo huo, Zungu alisema kuwa jina la Rais halipaswi
kutajwa kwa dhihaka, halaumiwi wala hatakiwi kusemwa kama alivyofanya
Peneza.
Alimtaka mbunge huyo kuuliza utendaji wa mawaziri kwa kuwa kanuni inawataka wabunge kutohoji utendaji wa Rais ndani ya Bunge.
“Jina
la Rais halitumiwi kwa namna ulivyokuwa unalitumia na kwa hiyo,
nayafuta maneno yote kwenye hansard (kumbukumbu rasmi za Bunge),”
alisema.
Hata hivyo, baada ya kupewa nafasi ya kuendelea kuchangia, Peneza aliendelea kusema juu ya kauli za Rais.
Kutokana
na hali hiyo, Mhagama alisimama tena kutaka kutoa taarifa lakini Zungu
alimzuia akisema: “Natumia kanuni ya 73 ukae chini hutazungumza tena.”
Wabunge
wengine waliochangia walitaka Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura),
kuongezewa mgawo wa fedha za bajeti kwa kuwapa nusu ya fedha za Wakala
wa Barabara (Tanroad) ili kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Mbunge
wa Lulindi, Jerome Bwanausi (CCM), alisema kama Tarura haijaongezewa
bajeti yake, utakuwa ni wakala ambao umeanzishwa lakini haujaleta tija.
“Sasa
hivi wakala huu umeazima watumishi kutoka halmashauri, wapewe watumishi
wao na fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara ili ziweze kupitika,”
alisema.
Mbali
na Mbunge huyo wabunge wengine waliochangia sula hilo ni pamoja na
Magdalena Sakaya (Kaliua-CUF), Livingstone Lusinde (Mtera- CCM), Fred
Mwakibete (Busokelo-CCM) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini - CUF).
chanzo:Mpekuzi.
Comments