Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh,
amekosoa hatua ya serikali kutoa majibu juu ya taarifa za ukaguzi wa
hesabu zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAOT).
Amesema
hoja za ukaguzi hazitolewi na mkaguliwa bali mwenye mamlaka ya kufanya
hivyo ni CAG mwenyewe baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa mapendekezo
yake.
Mapema
wiki hii, serikali ilianza kujibu hoja za ukaguzi za CAG kutokana na
taarifa ya ukaguzi wa taasisi za umma, huku ikisisitiza kuwa inafanya
hivyo kwa kuwa imepewa jukumu hilo kikatiba.
Utoah
ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu ambayo inalenga
kuhamasisha uwajibikaji na utawala bora nchini, alisema hayo jana katika
semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo wabunge wa kamati tatu za
bunge, mjini hapa.
Kamati
hizo ni za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
na ile ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC).Alisema inaonekana sasa hivi
hakuna uelewa mzuri kwa Watanzania kuhusu Ofisi ya CAG na majukumu yake.
“Ofisi
ile ipo kikatiba. CAG ana jukumu la kukagua mapato na matumizi yote ya
serikali na ni jukumu lake kuuambia umma wa Watanzania aliyoyaona, hivyo
niseme tu kwamba kuna utaratibu wa yeye kutengeneza hoja za ukaguzi na
kutoa hoja za ukaguzi,”alisema.
Alisema
inaweza kutokea CAG akaridhishwa na utekelezaji wa mapendekezo yake
baada ya uhakiki ndipo hoja ya ukaguzi inafutwa kwenye daftari la hoja
za ukaguzi.
Aidha,
alisema kuwa anatambua kamati hizo msingi wa kazi yake ni usimamizi na
uwajibikaji. Kutokana na jukumu hilo, kuna umuhimu wa kuelewa fika
katika ripoti zenyewe kitu gani kinazungumzwa na kuna umuhimu wa kufanya
hivyo.
“Madhumuni
ya mafunzo haya ni taasisi hii kujitambulisha rasmi kwa kamati za bunge
zinazoshughulika na usimamizi na uwajibikaji wa serikali ambapo ndio
jukumu kubwa la taasisi yenyewe hii,”alisema Utoah.
Alisema katika semina hiyo watazungumzia pia mambo ya uwajibikaji yaliyojikita kwenye ripoti ya CAG.
Naye
Mwenyekiti wa PIC, Raphael Chegeni, alisema taasisi hiyo ina watu
waliobobea kwenye masuala ya usimamizi wa fedha na itawawezesha kujua
namna ya kusimamia serikali.
“Pia
kutambua sisi tuna mchango gani wa kuhakikisha rasilimali za taifa
zinatumika vizuri. serikali ya awamu ya tano imejikita kuhakikisha
kunakuwa na matumizi mazuri ya rasilimali fedha,” alisema.
Alisema serikali imewekeza zaidi ya Sh. trilioni 48 hivyo ni lazima ipate mrejesho kwenye uwekezaji wake.
Naye, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo na kutambua wajibu wao.
Alisema
kamati ndiyo kiungo kati ya Bunge na serikali kwa ajili ya kuona fedha
za umma zinatumikaje na maofisa masuhuli wanahojiwa vipi.
“Hizi
hoja za CAG zikishaletwa bungeni zinakabidhiwa, PAC ndiyo inakaa na
kuchambua na kuwaita maofisa masuhuli kutoa majibu ya hoja za CAG kwa
kamati kutokana na fedha walizopewa.
“Sasa
kazi ya CAG anaenda kufanya uhakiki mara baada ya kuwasilishwa majibu
ya hoja husika ili kama hoja inafungwa ndiyo inafungwa au kama haifungwi
tunaendelea,”alisisitiza.
chanzo:Mpekuzi.
Comments